Ruto ampigia simu Uhuru na kumshauri atulize boli
BAADA ya kuhofia kile wadadisiuasi unaoweza kutokea Mlima Kenya , kufuatia malalamishi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya utawala wake Rais William Ruto amechukua hatua za kutuliza hali.
Hii ni kufuatia hisia kuwa malalamishi ya Bw Kenyatta na Bw Gachagua yanaweza kuchochea uasi Mlima Kenya dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.
Bw Gachagua na Bw Kenyatta ndio viongozi wakuu wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya, na malalamishi yao ya hivi majuzi dhidi ya serikali, wadadisi wanasema, yanaweza kusababisha uasi ambao haujawahi kushuhudiwa kutoka eneo hilo lililo na wapiga kura wengi.
Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed jana alisema, Rais Ruto alizungumza na mtangulizi wake kuhusiana na malalamishi ya kunyimwa pesa za bajeti ya ofisi yake.
“Rais Ruto ameunda kikosi, chini ya Mkuu wa Utumishi wa Umma (Felix Koskei), kushughulikia mara moja masuala yote yaliyoibuliwa, ikiwa ni pamoja na eneo la ofisi ya Rais mstaafu na yanayohusu wafanyakazi wa ofisi yake,” Bw Mohamed alisema.
Kabla ya malalamishi ya Bw Kenyatta, Naibu Rais Gachagua alikuwa ameshutumu baadhi ya viongozi wandani wa Rais Ruto kwa kupanga njama kumhujumu.
Mnamo Jumapili, alieleza hadharani changamoto ambazo amekuwa akikumbana nazo kwenye usafiri kufuatia wiki kadhaa za madai kwamba, amenyimwa ndege ya kijeshi.
“Mheshimiwa, nataka kukuomba radhi kwa kuchelewa kufika. Mimi si mtu aliye na nidhamu. Nilikuwa na changamoto katika mipango yangu ya usafiri na nilikwama kati ya Longonot na Naivasha kwa takriban saa mbili,” alisema Naibu Rais ambaye alifika katika hafla ya rais Nakuru kwa helikopta ya kibinafsi.
Lakini masaibu ya Gachagua yalifafanuliwa baadaye na mwandani wake, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ambaye alikashifu wazi wazi utawala wa Ruto kwa kumdhulumu Bw Gachagua.
Mwezi uliopita, Gachagua alihusisha hadharani baadhi ya washirika wa rais na masaibu yake, nao wakamkosoa vikali.
“Baadhi ya wanasiasa wachache walio karibu na Rais wanataka kuingilia siasa za Mlima Kenya ili kupigana nami. Siasa za Mlima Kenya ni ngumu sana na tunachochukia ni usaliti. Kama Mlima Kenya, hatujawahi kuingilia siasa za Bonde la Ufa na tunastahili heshima,” Naibu Rais alisema huko Uasin Gishu, kaunti ya nyumbani ya rais.
Lakini huku mvutano kati ya rais na washirika wa naibu wake ukiongezeka, Jumatatu, Rais mstaafu Kenyatta alielezea masaibu yake mikononi mwa utawala wa Rais Ruto.
Kupitia kwa msemaji wake, Bi Kanze Dena-Mararo, Bw Kenyatta alimshutumu Rais Ruto kwa kukataa kulipia afisi yake na kumnyima bajeti ya miaka miwili ya kifedha ya takriban Sh1.1 bilioni.
Wadadisi wanasema malalamishi ya Bw Kenyatta na Naibu Rais yanalenga kushawishi eneo la Mlima Kenya na kuvuruga utawala wa Ruto.
Jumanne, Gavana Kahiga alitaja unyanyasaji wa Gachagua na Uhuru kama njama ya kuhujumu eneo la Mlima Kenya.
“Mbona Mheshimiwa Raila Odinga na Mheshimiwa Kalonzo Musyoka, hawalalamiki kuhusu pensheni yao?
“Ingawa inaweza kutokana na sababu za kweli, inaonyesha ubaguzi wa hali ya juu,” Bw Kahiga aliambia Taifa Leo. Alisema ingawa Kenyatta “huenda alikosea serikali ya sasa, anastahili malipo yake ya kustaafu ambayo ofisi yake inapaswa kupata kisheria.
Mbunge wa Embakasi ya Kati, Benjamin Gathiru alisema anayopitia Bw Gachagua na Bw Kenyatta hayafai kwa kiongozi yeyote wa hadhi yao.
“Mbaya zaidi, inaungwa mkono na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya,” alilalamika mbunge huyo.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Bw Martin Oloo anahoji kuwa chochote kinachompata Naibu Rais na Rais huyo mstaafu ni “kuanzisha uasi na siasa za chuki.”
Mchanganuzi mwingine Bw Herman Manyora anasema kuwa, kumnyima Bw Kenyatta marupurupu yake halali ya kustaafu, na kwa kumnyanyasa wazi Naibu Rais Gachagua “Serikali ya Ruto inaalika uhasama mkubwa” kutoka lenye umoja la Mlima Kenya.
“Matokeo kwa Ruto yanaweza kuwa mabaya,” Bw Manyora anaongeza.
Lakini Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah anasema malalamishi hayo kama njama iliyoratibiwa vyema na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya kuyumbisha utawala wa Ruto.
Akiongea huko Kiambaa, kaunti ya Kiambu siku ya Jumatatu, mbunge huyo wa Kikuyu alimkashifu Naibu Rais, na kuapa kutomwacha rais Ruto kumuunga mkono.