Makala

Mbunge adai Nupea inatumia kifua kujenga kiwanda cha nyuklia Uyombo

June 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Kilifi Kaskazini Owen Baya amedai shirika la kawi ya nyuklia (Nupea), limekuwa likiwatenganisha wakazi wa kijiji cha Uyombo katika wadi ya Matsangoni, ambapo mtambo wa kutengeneza umeme kupitia nyuklia unatarajiwa kujengwa.

Kulingana na Bw Baya, wananchi na hata serikali haijalipatia shirika hilo, ambalo kwa Kiingereza ni Nuclear Power and Energy Agency, idhini ya kuweka mtambo wa kuzalisha kawi ya nyuklia katika kijiji cha Uyombo kwani hata halina ardhi na iliyoko ni ya wananchi.

Bw Baya alisema kuwa licha ya kuwa nchi ya Kenya inajitayarisha kupunguza gharama ya umeme kupitia nyuklia, shirika la Nupea halijakuwa tayari kutekeleza mradi wa aina hiyo vilivyo.

Akizungumza wakati wa kuzinduliwa rasmi kwa bwalo (dining hall) katika Shule ya Upili ya Majaoni, mbunge huyo alisema kuwa Nupea ilishindwa kutekeleza wajibu muhimu wa kuandaa vikao vya umma mashinani kujadili pamoja na wananchi swala hilo nyeti.

“Nataka kuwaambia wakazi wa Matsangoni wawe na imani na mimi kwa sababu haya maneno ya nyuklia tutamalizana nayo. Hatutakubali kujenga mtambo hapa ambao utaathiri uchumi wa eneo hili,” akasema Bw Baya.

Mbunge huyo alisema kuwa aliwashauri maafisa kutoka katika shirika la Nupea ambao walipewa jukumu la kutafuta pahala pa kujenga mtambo wa nyuklia nchini kuwa Katiba ya 2010 inasema kuwa ni lazima mwananchi ahusishwe kikamilifu katika maswala ya maendeleo ikiwemo kabla kuanzishwa kwa miradi.

“Niliwaleta Nupea mashinani kukutana na wananchi na nikawaambia wafanye vikao na jamii vilivyo kwa sababu mtambo wa nyuklia ni hatari na hatutaki kuwa na ile hali ya kuwa jamii iliyo na watu wengi inaunga mkono na ile ya wachache inapinga kwani iwapo kutatokea mkasa, wakazi wote wataathirika,” akasema.

Alisema aliwashauri Nupea waende mashinani ili kuungwa mkono na wananchi wote ama pia waukatae mradi huyo kwa pamoja.

“Niliwajulisha maafisa wa Nupea kwa wanajamii na kuwaachia kujukumu hilo ili walitekeleze vikamilifu na nikaweleza kuwa nitaunga mkono uamuzi wa wananchi,”akasema.

Kulingana na Bw Baya, hatua yake kuwapeleka mashinani na kuwatambulisha kwa jamii ilikuwa nafasi nzuri ya maafisa hao kuwapa wananchi habari sahihi na za ukweli na kuwashawishi kuwa inawezekana kuwepo kwa mtambo wa umeme wa nuklia pamoja na wao.

“Kutokea 2021 hadi wa leo hawajanipa jibu la kuridhisha kuwa walifanya vikao na wananchi ila wamewaganya na kuwabagua wananchi, na wanaongea tu na wale ambao ni marafiki wao na kuwagandamiza wale ambao sio marafiki wao,” akasema.

Alidai kuwa wapo baadhi ya maafisa wa Nupea wanaodhania kuwa wanaweza kutumia uongozi wa kiimla kuzigonganisha jamii ili kukusuma mradi huo wa nyuklia.

“Nupea walianza kupeleka watu wachache wanaokubaliana nao katika hafla hotelini na kuwakandamiza wapinzani ikiwemo kutumia maafisa wa utawala kuwahangaisha wale ambao hawakukubaliana nao,” akadai.

Bw Baya alidokeza kuwa alikataa kusafiri kuenda ng’ambo kutembelea mitambo ya nyuklia kwani sauti yake haingekuwa na maana ama nguvu yoyote katika kutoa uamuzi kuhusu mradi huo nyumbani.

Badala yake, alishauri Nupea kuwachukua wakazi ambao wataathirika moja kwa moja na mradi huo ili waende kujionea wenyewe.

“Nupea walipuzilia mbali mawaidha yangu na kuchukua maafisa wa utawala , afisi ya gavana wa Kilifi, Mwakilishi wadi na wao wakaenda Ghana,”akasema.

Baadhi ya walioenda ni Kamshina wa Kaunti ya Kilifi Josephat Biwot, mwakilishi wadi wa Matsangoni Bw Hassan Mohamed.

“Nupea imeshindwa kutoa ripoti muhimu ikiwemo ya ukaguzi wa mazingira na ile ya kazi zao ambazo wamejitolea kwa jamii(CSR) na ile ya vikao vya jamii mashinani ambayo ilikuwa baadhi ya masharti aliyowapa,” akasema.

Mbunge huyo aliendelea kusema haifai Nupea kuanza kujenga mnara wa kuchukua ripoti za hali ya anga katika shule ya upili ya Uyombo kujua iwapo mtambo wa nuklia unafaa katika sehemu hiyo ama la kwa hawajaweza kutoa ripoti hizo muhimu ambazo zingesaidia kujua iwapo jamii imekubali mradii huo ama la.

“Niliambia Nupea kuwa muda wenyu umeisha , tumewapa muda wa kutosha kutokea 2021 kuongea na wananchi na kuleta ripoti hadi sasa hawana la kutuonyesha,” akasema.

Bw Baya alisema kuwa ikiwa kuwepo kwa mtambo ya nuklia utaathiri mazingira na sekta ya utalii pakubwa na hata pia elimu.

Alitoa mfano na kusema hata shule hiyo ya upili ya Majaoni ambayo ina takribani wanafunzi 1400 kwani itahamishwa.

“Tuliwapa nafasi ya kufanya vikao na jamii wakashindwa, tukawapa nafasi ya kushirikisha jamii wakafeli na iwapo wameshindwa kutekeleza mambo rahisi ambayo tuliwapa, watawezaje kushughulikia nyuklia?” akauliza.

Bw Baya alisema kuwa amewasilisha mswada Bungeni wa kutaka kuvunjwa kwa shirika la Nupea na kulifanya kuwa kitengo kidogo katika Wizara ya Kawi na kuomba wabunge wenzake kummuunga mkono.

“Nupea haitakuwa na biashara yoyote Kilifi na wakitaka kufanya mambo yao, waende katika kaunti nyingine lakini Kilifi haiko tayari. Utalii hauwezi kukakaa pamoja na nyuklia na kwa sababu hiyo, nataka kusema kuwa poleni, niko kwa serikali lakini hatutakubaliana kwa swala hili,” akasisitiza.

Jumatatu ya juma lililopita, Kamishina wa Kaunti ya Kilifi Josephat Biwott na msafara wake wa kamati ya usalama walilazimika kuahirisha kikao cha baraza kilichokuwa kimeandiliwa katika soko la Uyombo baada ya wananchi waliojawa na ghadhabu kudinda kuhudhiria kwa madai kuwa hawakuwa na haja ya mtambo wa nyuklia na kwa hivyo hawakuwa na sababu ya kusikiliza viongozi hao.

Wananchi hao waliokuwa wamepiga kambi katika soko la Uyombo na kuziba barabara pia waliwafurusha maafisa wa Nupea waliokuwa wamendamana na Bw Biwott kwa madai kuwa waliwatumia maafisa wa polisi kuwapiga huku wengine wao wakiendelea kuuguza majeraha ya mwili.

Bw Biwott aliwaeleza kuwa mkutano huo ulikuwa umeandaliwa ili kujadili maswala ya mradi wa nyuklia na ungewapa wakazi hao nafasi nzuri ya kutoa malalamishi yao moja kwa moja kwa maafisa wa Nupea na serikali.

Kabla ya Bw Biwot na msafara wake kuwasili, Naibu Kamishna wa Kilifi Kaskazini Bw Samuel Mutisya alikuwa na wakati mgumu kuwashawishi wakazi hao wa Uyombo kuhudhuria kikao hicho baada ya wao kudai kuwa chifu wa eneo hilo na mzee wa mtaa waondoke kwani walichangia kupigwa kwao na polisi.

Ilibidi viongozi hao kuondoka kwa pikipiki huku wanachi hao wakiwazoma.

Hata hivyo, bado walidinda kuhudhuria mkutano licha na kutaka kuandaliwa mkutano siku nyingine.

Matamshi ya mbunge huyo yanawawadia baada ya wakazi wa Uyombo wakiongozwa na Bw Mwagombe Mwagambo almaarufu Ririri kumkosoa vikali na kudai kuwa alikuwa anawahadaa.

Bw Ririri alisema kuwa Bw Baya amekuwa akiwahepa na amekosa kuzungumzia swala hilo kwa muda.

“Sasa yeye anapinga na ni yeye alileta huo mradi. Sisi tunafunikwa macho kumbe watu wana miradi yao ambayo wanaendeleza. Hatutaki nyuklia,” akasema Bw Ririri.

Hapo mwanzo, wakazi hao waliandamana kupinga kujengwa kwa mnara katika shule ya Uyombo.

Mzozo unaondelea kuhusu mradi wa nyuklia umeathiri pakubwa masomo katika shule ya msingi ya Uyombo/Maweni kwani imegeuka kuwa uwanja wa vita baina ya polisi na wakazi wakirushiana risasi, vitoa machozi na mawe.

Hali hiyo iliwalazimu walimu kuwaficha wanafunzi katika darasa moja kwa kuhofia kujeruhiwa huku watoto wengine wakikimbilia msituni.

Shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 147 lakini kufikia Jumatatu ya wiki jana, idadi hiyo ilikuwa imepungua.

Kitengo cha chekechea katika shule hiyo ndicho kimeathirika pakubwa.

[email protected]