Makala

Biashara ya vipakio vya avokado za ng’ambo

June 12th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

KENYA inaongoza katika uzalishaji wa maparachichi (Avokado) Afrika, ikiorodheshwa kidedea kuuza zao hilo nje ya Bara. 

Ulimwenguni, inashikilia nafasi ya tano Mexico ikiwa juu ya jedwali.

Kando ni vigezo faafu kitaalamu katika uzalishaji wa avokado, upakiaji pia ni nguzo muhimu kuzingatia kuhakikisha mazao yanatua sokoni yakiwa freshi.

Miundo msingi ya usafirishaji inajumuisha vipakio na mbinu ya kuyasafirisha – kwa njia ya ndege au meli.

Muhimu zaidi, ni kiwango cha nyuzijoto kinachopendekezwa kikiwa kati ya sentigredi (°C) 4 hadi 6.

Vipakio ni nguzo muhimu katika kuafikia vigezo hivyo, na Shri Krishana Overseas Ltd (SKL) ni kati ya wadauhusika kuhakikisha maparachichi yanafika masoko ya ng’ambo yakiwa shwari.

Mwenyekiti wa Shri Krishana Overseas Ltd (SKL), Dkt Sonvir Singh, akielezea kuhusu uundaji wa makatoni ya kusafirisha avokado ng’ambo, wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024, yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Ikiwa na makao yake jijini Nairobi, kampuni hiyo inaunda makatoni ya kusafirisha avokado kwa kutumia malighafi ya ndani kwa ndani.

“Malighafi tunayotumia kuyatengeneza ni ya humu nchini,” Mheshimiwa Dkt Sonvir Singh, Mwenekiti wa Muungano wa SKL anasema.

Bagasse, masalia ya vipande vya miwa au mtama, inapokamuliwa kupata sukari ama juisi, ni mojawapo ya malighafi.

Uundaji wa vipakio hivyo, Dkt Sonvir anasema unalenga kuboresha soko la maparachichi kuhakikisha yanafika ng’ambo yakiwa na uhalisia wake.

Mataifa ya Bara Uropa, China, Dubai, na Milki za Kiarabu (UAE), ndio wanunuzi wakuu wa maparachichi ya Kenya.

Vipakio vya Shri Krishana Overseas Ltd, Dkt Sonvir anaelezea vimetengenezwa kiasi kuwa vinadumisha uhalisia wa matunda na haviharibiwi na maji wala unyevuunyevu.

“Tunashirikiana kwa karibu na kampuni na mashirika yanayouza avokado nje ya nchi, la mno likiwa ni kuhakikisha wakulima wa mapato ya chini na kadri wananufaika kupitia bei nafuu ya makatoni,” anafafanua.

Katoni ya kusafirisha avokado masoko ya ng’ambo. PICHA|SAMMY WAWERU

Bei, kwa mfano, katoni ya kilo 4 Dkt Sonvir anafichua kwamba inachezea kati ya Sh72 hadi Sh85.

Shri Krishana Overseas Ltd imekuwa kwenye biashara ya utengenezaji wa vipakio vya avokado kwa zaidi ya miaka 15, afisa huyo akidokeza kwamba pia huunda vile vya mafuta ya matunda hayo.

Kampuni hiyo ilikuwa miongoni mwa washirika waliohudhuria Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024, yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi, Mei 7 hadi 10.

Yakiwa ni Makala ya Nne, yaliandaliwa na Chama cha Ushirika cha Maparachichi Kenya, ndicho Avocado Society of Kenya.

Mheshimiwa Dkt Sonvir Singh, Mwenyekiti Shri Krishana Overseas Ltd (SKL) wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024, yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi akifungua katoni ya kupakia maparachichi. PICHA|SAMMY WAWERU

Mashirika ya kiserikali; Agriculture and Food Authority (AFA) na Horticultural Crops Directorate (HCD), ndiyo hupiga msasa maparachichi yanayouzwa nje ya nchi.

Kulingana na data za AFA, kiwango cha shamba kinacholimwa avokado kimeongezeka kutoka Hekta 26,561 (2021) hadi Hekta 27,807 mwaka wa 2022.

Kiwango cha uzalishaji nacho, kimepanda kutoka Tani Metri (MT) 432, 969 mwaka 2021 hadi 455,279 MT (2022), hilo likiashiria ongezeko la asilimia 5.2.

Mwaka 2022, wakulima walitia kibindoni Sh12.6 bilioni, ikilinganishwa na 2021 Sh12.4 bilioni.


Dkt Sonvir Singh, Mwenyekiti Shri Krishana Overseas Ltd (SKL) na mmoja wa maafisa wake wakati wa Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024, yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi akijadiliana na mfanyakazi mwenza kuhusu katoni ya kupakia maparachichi. PICHA|SAMMY WAWERU