Habari za Kitaifa

Wakenya kuishi maisha marefu — miaka 10 zaidi kuliko kawaida, ripoti yasema

June 13th, 2024 2 min read

MARY WANGARI

WAKENYA sasa wataishi maisha marefu zaidi huku umri wa maisha yao ukikadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya miaka kumi, ripoti mpya imeonyesha.

Maisha ya wanawake nchini yameongezeka kwa jumla ya miaka 16 nao wanaume kwa miaka 14 zaidi katika kipindi cha miaka mitano, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Baraza la Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (NCPD).

Umri wa watu wazima kwa wanawake umeongezeka hadi 67 kutoka 51 huku umri wa wanaume ukipanda kutoka 47 hadi 67, inaeleza Nakala Nambari 1 ya 2023 kuhusu Sera ya Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu kwa Ustawishaji Maendeleo Nchini.

Wanawake wamekadiriwa kuishi maisha marefu zaidi ikilinganishwa na wanaume huku umri wa maisha ya watu wazima kwa jumla ukiimarika kwa kasi kati ya 1969 na 2019, inaeleza ripoti hiyo iliyozinduliwa wiki iliyopita.

Kulingana na Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi Nchini 2019,” wanawake huishi maisha marefu kuliko wanaume ambapo kwa kila wanaume 1,000 wanaofikisha umri wa miaka 15, wanaume wapatao 341 hawafikishi umri wa miaka 60 ikilinganishwa na wanawake 212.”

“Kiwango cha vifo vya watu wazima ni kiashiria muhimu cha kuwezesha kutathmini kikamilifu mtindo wa vifo katika jamii. Idadi ya vifo miongoni mwa wanawake imekuwa ikipungua kwa kasi zaidi ikilinganishwa na vifo vya wanaume waliokomaa,” inaeleza ripoti.

Wazee wenye umri wa miaka 60 kwenda juu ndilo kundi linaloongezeka kwa kasi zaidi nchini, linaashiria toleo la tano la Nakala hiyo ya Msimu linalochapishwa kila baada ya miaka 10.

Katika muda wa mwongo mmoja uliopita, idadi ya watu wazee imepanda kwa kasi kwa asilimia 42 hadi 2,740,555 kutoka 1,926,051 kati ya 2009 na 2019 huku sehemu kubwa ya wazee nchini wakiwa wanawake, asilimia 55.

Japo umri wa wanajamii umeimarika nchini, ripoti hiyo inaashiria kuwa “Kenya ingali inakabiliwa na viwango vya juu vya maradhi yasiyo ya kuambukizana, matatizo ya uzazi, changamoto zinazohusu lishe na vifo vya watoto wachanga licha ya mzigo wa maradhi kuhamia magonjwa yasiyo ya kuambukizana na majeraha.”

Mkurugenzi wa NCPD, Mohamed Sheikh, akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo alifafanua kuwa,” hali hii ya umri wa maisha kuongezeka kwa kasi ina athari kwa mikakati ya kulinda wanajamii chini maadamu umri rasmi wa kustaafu Kenya ni miaka 60.”

Ripoti hiyo imeorodhesha kuzorota kiafya, hali duni ya mapato, usalama na ulinzi wa jamii, Ukatili, Dhuluma na Kutelekezwa (VAN) na unyanyapaa dhidi ya wazee, kama changamoto kuu zinazowakabili wazee.

“Zaidi ya nusu ya wazee nchini wanaishi katika uchochole na wanajumuisha kundi la watu fukara zaidi nchini. Sehemu ya wazee wanaopokea msaada nchini inakadiriwa kuwa asilimia 24.6.”

Gonjwa la ukimwi limesalia chanzo kikuu cha vifo miongoni mwa watu wazima ambapo walio na umri kati ya 15-49 wanaishi na virusi hivyo.

Wazee wenye umri kati ya 60-64 wapo hatarini zaidi ya kufa kutokana na kiharusi na maradhi ya moyo huku homa ya mapafu na matatizo yanayohusu ujauzito yakichangia zaidi vifo vya wanaume na wanawake wenye umri kati ya 30-34 mtawalia.