Tambua kwa nini msitu wa Boni tatizo si usalama pekee
NA KALUME KAZUNGU
WENGI wanapotajiwa kuuhusu msitu mkuu wa Boni, Kaunti ya Lamu, kinachowajia fikirani mwao mara nyingi huwa ni utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.
Hili linatokana na kwamba kwa karibu miaka kumi sasa, msitu huo umeibuka kuwa ngome kuu inayotumiwa na magaidi hao wenye makao makuu katika nchi jirani ya Somalia kujificha.
Ni kutokana na hilo ambapo msitu wa Boni umekuwa ukigonga vichwa vya habari, hasa pale serikali ya kitaifa ilipoafikia kuzindua operesheni ya kiusalama kwa jina linda Boni.
Operesheni hiyo inayotekelezwa na Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF) kwa ushirikiano na vitengo mbalimbali vya polisi ilianzishwa mnamo Septemba 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo.
Ila wasichokijua wengi ni kuwa utovu wa usalama unaosababishwa na Al-Shabaab siyo changamoto ya pekee inayokumba wakazi na walinda usalama wanaohudumu ndani ya msitu wa Boni.
Msitu huo bado umesheheni changamoto zingine chungu nzima, ikiwemo miundomsingi duni, hasa ile ya usafiri.
Ni msitu wa Boni ambako barabara zote ni za mchanga na vumbi wakati wa kiangazi ilhali zikigeuka kuwa matope na vidimbwi tele vya maji punde kunaposhuhudiwa mvua.
Ni hali hiyo duni ya barabara za msitu wa Boni ambayo mara nyingi imeacha walinda usalama wakihangaika, hasa wakati magari yao yanapozikika mchangani au kukwama matopeni wakati wanapotekeleza doria zao za kila siku.
Hali hiyo huwaweka walinda usalama hao kwenye hatari ya kushambuliwa na magaidi kwani wamekuwa na hulka ya kujificha kandokando ya vibarabara vya msitu wa Boni na kisha kuchomoka ghafla na kushambulia, kujeruhi au hata kuua walinda usalama.
Hali hiyo duni ya barabara za msitu wa Boni, ikiwemo kusheheni kwa mchanga pia imetoa mwanya kwa Al-Shabaab kuzika vilipuzi vyao vya ardhini (IED) na kuishia kuwaangamiza walinda usalama.
Kati ya 2014 na 2024 kwa mfano, mamia ya walinda usalama, ikiwemo KDF na polisi wamejeruhiwa au hata kuuawa na magaidi wa Al-Shabaab kupitia kutega vilipuzi kwenye vijibarabara vya msitu wa Boni.
Kwenye msitu wa Boni, kuna sehemu nyingi ambazo hata mawimbi ya mawasiliano ya simu, hasa zile za mkononi hakuna.
Hilo limekuwa likiwaacha walinda usalama gizani wakati wanapovamiwa na maadui kwani huwanyima fursa ya kuwasiliana na wenzao maeneo mengine ili kuitisha msaada wa dharura au kuongeza nguvu punde kunapotokea uhitaji wa ghafla.
Baadhi ya maafisa wa usalama, ikiwemo KDF na polisi waliohojiwa na Taifa Leo na kudinda kutajwa majina yao kutokana na kwamba hawajapewa mamlaka ya kuzungumza kwa vyombo vya habari, walikiri kuwa kuhudumu maeneo ya msitu wa Boni ni sawasawa na mja kuyatoa maisha yake mhanga.
Maafisa hao wanashikilia kuwa unapohudumia eneo la msitu wa Boni, mja lazima ajihami na moyo wa simba na wala hakuhitajiki mioyo dhaifu au minyonge eneo hilo. “Hapa mja lazima awe ni mwenye kujitolea na kukubali kwamba maisha yanaweza kumponyoka wakati wowote. Yaani kuhudumu hapa ni sawa na kuyatoa maisha yako mhanga,” akasema afisa huyo.
Changamoto nyingine inayokabili walinda usalama wanaohudumia maeneo ya msitu wa Boni ni jinsi msitu huo ulivyo mkuu na uliozagaa na kutwaa maili au kilomita nyingi.
Ikumbukwe kuwa msitu wa Boni unapatikana kwenye kaunti za Lamu, Tana River na Garissa, ambapo pia huishia kugusagusa au kuingia kabisa nchini Somalia.
Msitu wa Boni una ukubwa upatao kilomita karibu 1,500 mraba.
Hilo limechangia walinda usalama mara nyingine kukosa kuwadhibiti maadui, hivyo kuwapata Al-Shabaab wakipenya na kuyafikia makazi ya binadamu kutekeleza mashambulio na mauaji.
“Kutembea ndani ya msitu wa Boni huku ukiwa umevalia viatu hicho tayari huwa ni kibarua kigumu na cha ziada. Ardhi ya msitu wa Boni huwa sehemu nyingi ni majimaji na matope. Pia kuna mito hatari msituni. Ila tunajikaza ilmuradi tulilinde eneo zima la Boni na watu wake na pia kuidhibiti Kenya dhidi ya kulengwa na maadui kutoka nje,” akasema afisa mwingine wa usalama.
Boni pia ni eneo pweke kwani hata maduka ya kujinunulia bidhaa, vituo vya afya na huduma nyingine za kimsingi havipatikani.
Hii inatokana na kwamba zahanati nyingi za msitu wa Boni zilifungwa tangu 2014 kufuatia kulengwa kwa vituo hivyo vya afya na Al-Sabaab ambao walikuwa wakiiba dawa na kisha kuteketeza zahanati hizo.
Miongoni mwa zahanati zilizofungwa ni Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe.
Aidha juhudi za maafisa wa usalama katika kukabiliana na Al-Shabaab zimesaidia pakubwa kudhibiti usalama, hivyo kupisha zahanati kama vile Kiangwe kufunguliwa mnamo 2022, ambapo wananchi wa mbali na karibu wamekuwa wakihudumiwa kimatibabu.
Ni juma hili pia ambapo zahanati ya kijiji cha Mangai ilifunguliwa rasmi baada ya kufungwa kwa miaka 10 kufuatia ukosefu wa usalama msituni Boni.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo hata hivyo waliwashukuru walinda usalama, hasa KDF na vitengo vya polisi ambao wamejitolea kuhudumia wananchi wa jamii ya wachache ya Waboni vijijini mwao bila kuzingatia changamoto tele zilizoko eneo hilo.
Bi Asha Ali, mkazi wa Mararani, alisema tangu operesheni ya Linda Boni kuzinduliwa 2015 imesaidia pakubwa kwani kumeshuhudiwa kuimarika kwa usalama kila kukicha vijijini mwao.
“Ninawapongeza walinda usalama wetu kwa kupuuzilia mbali uoga na kukubali wito wa wao kuhudumu ndani ya msitu wa Boni. Juhudi zao ndizo zinachangia amani na utulivu kudumu eneo hili. Tusiogope, tusihofu,” akasema Bi Ali.