Oliech arejea KPL, Gor kumlipa Sh350,000 kwa mwezi
Na CECIL ODONGO
STRAIKA wa zamani wa timu ya taifa Harambee Stars Dennis Oliech atakuwa mchezaji anayelipwa mshahara wa juu zaidi katika ligi ya KPL baada ya kukamilisha uhamisho wake kuichezea Gor Mahia.
Nyota huyo atatambulishwa rasmi kwa mashabiki Januari 9 katika uga wa michezo wa Moi mjini Kisumu wakati mabingwa hao watetezi wa KPL watakapomenyana na Posta Rangers kwenye mechi ya ligi ya KPL.
Oliech atakuwa akitia mfukoni Sh350,000 kila mwezi kulingana na kandarasi ya mwaka mmoja na nusu aliosaini baada ya kuridhisha kocha Hassan Oktay wakati wa majaribio mara mbili aliyoyashiriki na Gor.
Mwanadimba huyo pia atatia mfukoni kitita cha uhamisho cha Sh3.5milioni ambacho kitalipwa kwa awamu mbili.
“Nimefanya mazoezi kabambe na Gor Mahia na nimefanikiwa. Nafurahi kocha ameamua kunisajili na naahidi kwamba nitatesa sana nikirejea kusakatia ligi ya KPL niliyoagana nao miaka mingi iliyopita,” akasema Oliech.
K’Ogalo wamekuwa wakikumbwa na tatizo la kuyafuma mabao langoni baada ya miguu ya washambulizi Jacques Tuyisenge, Francis Mustapha na Ephrem Guikan kuingia kutu na kukosa kutambisha timu kwenye michuano ya CAF na KPL.
Vile vile kudidimia kwa fomu ya viungo Humphrey Mieno na Earnest Wendo kumechangia pakubwa mastraika hao kukosa kupokezwa mipira na kuwalazimu kurejea nyuma kujitafutia mipira na kupokezana krosi.