Afueni kwa Wakenya bei ya mafuta ikishuka tena
NA CHARLES WASONGA
NI afueni kwa Wakenya baada ya serikali kwa mara nyingine kupunguza bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kati ya Sh3 hadi Sh6.08 kwa lita.
Kulingana na ratiba ya bei mpya iliyotolewa Ijumaa, Juni 14, 2024 na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (Epra), bei ya petroli imeshuka kwa Sh3, bei ya dizeli ikiteremka kwa Sh6.08 huku bei ya mafutataa ikishuka kwa Sh5.71 kwa lita.
Hii ina maana kuwa jijini Nairobi na viunga vyake, petroli itauzwa kwa Sh189.84, dizeli ikiuzwa Sh173.10 na mafuta taa yakinunuliwa kwa Sh163.05 kuanzia Juni 15, 2024 hadi Julai 15, 2024.
Kuanzia Mei 15, 2024 bei za petroli, dizeli na mafuta taa zimekuwa Sh192.84, 179.18 na Sh168.76, mtawalia jijini Nairobi.
“Bei hizi mpya zinajumuisha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) wa kima cha asilimia 16,” Mkurugenzi Mkuu wa Epra Daniel Kiptoo akasema kwenye taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari.
Mjini Mombasa na maeneo ya karibu, petroli itauzwa kwa Sh186.66, dizeli itauzwa Sh169.93 huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh160 kwa lita.
Hii ni kwa sababu Mombasa iko karibu na bandari ambako shehena za bidhaa hizo hupakuliwa baada ya kusafirishwa kwa meli kutoka mataifa ya Uarabuni.
Mjini Nakuru petroli, dizeli na mafuta taa yatauzwa Sh188.90, Sh172.54 na Sh162.57, kwa lita, mtawalia.
Na katika mji wa Eldoret bei za rejareja za bidhaa hizo zitakuwa Sh189.67 (petroli), Sh173.31 (dizeli) na Sh163.34, mtawalia.
Mjini Kisumu wateja watanunua bidhaa hizo kwa Sh189.66 (petroli), Sh173.31 (dizeli) na Sh163.34 (mafuta taa).
Bei ya bidhaa hizi zimekuwa zikishuka ndani ya miezi michache iliyopita kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kimataifa, haswa Dola ya Amerika.