Bambika

Shoo zilizobamba katika historia ya sanaa nchini Kenya

June 14th, 2024 3 min read

NA SINDA MATIKO

HISTORIA ya vipindi vya televisheni vilivyotikisa nchi itakapoandikwa, zipo shoo ambazo daima zitasalia kwenye kumbukumbu.

Ukiachia mbali shoo za maigizo kati ya shoo ambazo kila uchao zinazidi kupata umaarufu hapa nchini ni zile za Reality Show-kwa maana ya, shoo ambazo sio za kuigizwa.

Japo zipo ambazo zilikashifiwa kwa kueneza maadili yasiyo mema, zipo ambazo zilizosifiwa kwa kuwakosha watazamaji.

Kwenye makala haya, tunadadavua Reality Show zilizofanikiwa kujipatia umaarufu nchini.

Omo Pick a Box, KBC

Katika miaka ya 90 kama kulikuwepo na shoo iliyowakusanya Wakenya majumbani mwao kila Jumapili usiku, basi ilikuwa ni hii.

Kwa wana waliokulia miaka hiyo na wazazi waliolea enzi hizo, basi hakuna asiyeifahamu shoo hii.

Mpango wa shoo ulikuwa sio kuwashangalia washindani, ila kuwacheka washindani ambao walikuwa wanafanya maamuzi mabaya kwenye kuchagua OMO ama Box ambayo ilikuwa na zawaidi aina aina.

Kuna nyakati kuchagua Box kungemshindia mshindani zawadi nono nono na kuna wakati ungekosa. Tukio moja la shoo hiyo lisiloweza kusahaulika ni yule jamaa aliyechagua BOX badala ya Omo.

Licha ya jitihada za kumtaka abadilishe mawazo ikiwemo kukabidhiwa Sh30,000 ili abadiilishe msimamo, bado alikataa na kung’ang’ania Box.

Box ilipofunguliwa zawadi aliyokutana nayo mule ikawa ni sahani ya nyama choma.

Baada ya hapo zilizotokea shoo nyingi za namna hiyo kama vile ‘Who Want’s to be a Millionaire?’, ‘Who is Smarter Now’, ‘Zain Africa Challenge’ kati ya nyingi nyinginezo hamna iliyoweza kufikia umaarufu wa ‘Omo Pick a Box’.

Nairobi Diaries, K24

Ni Reality shoo iliyoundwa na Janet Mwaluda. Nairobi Diaries ilikuwa ndio reality ya kwanza kufuatilia na kuangazia maisha ya maceleb.

Lakini mfumo wake ulikuwa ni kuangazia maisha ya masoshiolaiti wa Nairobi.

Ni shoo iliyopata umaarufu kutokana kuwa wahusika wengi walikuwa na ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Lakini hata zaidi ni kutokana na zile drama na bifu walizoibua ndio zilichochea show kupata umaarufu.

Wife Material, YouTube

Ni shoo nyingine unayoweza kusema ilizua gumzo sana nchini kama Nairobi Diaries kutokana na drama iliyoibua.

Shoo hiyo iliyopeperushwa 2021 ilibuniwa na mchekeshaji Eric Omondi.

Shoo iliangazia pilkapilka za Eric kusaka mke hivyo aliweza kuishi na wanawake tofauti kumsaka yule mmoja.

Ni shoo iliyokutana na kashfa nyingi kutoka kwa Wakenya waliohisi iliendeleza udhalilishaji wa wanawake na pia ukosefu wa maadili kwa kuonyesha baadhi ya matukio ambayo yalipaswa kuwa ya faraghani.

Perfect Match, Ebru TV

Lazima utakuwa umekutana na viklipu vya vipindi vya shoo hii kwenye mitandao.

Shoo hii iliundwa lengo likiwa ni kuwakutanisha watu wawili wasiojuana ili waweze kuishia kuwa wapenzi.

Wahusika walikutanishwa kwenye mkahawa kupata chakula na wangejadili sifa wanazozipendelea kwa yule wanayesaka kuwa mwenza wao.

Mara nyingi wahusika waliishia kuzenguana kutokana na baadhi ya wahusika kuwa na matarajio ama sifa za kupitiliza walizokuwa wakizisaka kutoka kwa waliokuwa wanasaka kuwa wapenzi wao.

Perfect Match ilikuwa ni mwigo wa shoo sawia Tujuane iliyopeperushwa na KTN hapo awali.

Tujuane hata hivyo haikuonekana kuwa na hekaheka nyingi sana kama Perfect Match huku waandalizi wakishutumiwa mara kadhaa kwa kuigiza shoo kisha kudai ni Reality.

Slim Possible, Citizen TV

Hii ilikuwa ni shoo iliyowahusisha watu wanene tu. Washindani kadhaa walifanyiwa usaili wa kuingia kwenye droo ya shoo. Baada ya kufuzu walianza kushindanishwa kila wiki kwa muda wa wiki tano.

Mtihani ulikuwa mmoja tu, ni nani ambaye alipunguza kilo nyingi kufikia mwisho wa wiki.

Kila wiki walikuwepo washindani waliochujwa kwa kutegemea na uzito wao. Mwanzo wale ambao hawakuweza kupunguza uzito na kusalia na uzito waliokuwa nao wiki iliyopita lakini pili waliopunguza kilo chache.

Kutokana na ushindani mkubwa, washindani wengi walilazimika kubadilisha maisha yao hasa upande wa msosi lakini pia kujihusisha na mazoezi ili kuweza kupoteza kilo na kujihakikishia nafasi ya kupiga hatua hadi fainalini.

Mshindi wa Season 3, Clementine Mauka ni kati ya washindi waliopoteza kilo nyingi kwenye shindano.

Mauka alipoingia shindanoni alikuwa na kilo 147 ila kufikia mwisho wa wiki tano alikuwa amepunguza jumla ya kilo 40 na kuondoka na zawadi ya Sh1 milioni.

Ni shoo iliyovutia utazamaji mkubwa kutokana na mitihani waliokuwa wakipitia wahusika kupunguza unene.

The Real Housewives of Nairobi, Showmax

Unaweza kuifananisha na ila tofauti na ile, RHON haiangaziii maceleb tu, ila maisha ya mastaa wa kike ambao wamefanikiwa kimaisha.

Wanaishi maisha ghali, wanatesa mitaa lakini pia ni wanafamilia.

Sifa hizi ukiachia mbali umaarufu wa wahusika ndizo zimechangia RHON kupata umaarufu zaidi nchini. Kwa sasa shoo hiyo ipo katika Season yake ya pili.