Makala

2019: Bangi itahalalishwa Kenya mwaka huu?

January 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MIJADALA kuhusu iwapo bangi inapasa kuhalalishwa au la ilichipuza katika bunge la kitaifa na lile la seneti mwaka wa 2018.

Swali ni je, mjadala huu utazidi kutawala gumzo mitandaoni na kwenye vyombo vya habari mwaka huu?

Mbunge wa Kibra Ken Okoth alimwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akitaka asaidiwe kuandaa mswada unapendekeza kuhalilishwa kwa matumizi ya bangi nchini huku baadhi ya wenzake wakipinga pendekezo hilo.

Kwenye barua aliyowasilisha kwa afisi ya Bw Muturi mnamo Aprili 24, 2018 Okoth pia alisema mswada wake utalenga kuhalalisha ukuzaji wa mmea huo nchini na watu waliokamatwa kwa kosa la kutumia dawa hiyo ya kulevya waachiliwe huru.

“Mswada ninaupendekeza unalenga kuhakikisha kuwa upanzi na matumizi ya bangi unasimamiwa kisheria huku watoto wakilindwa dhidi ya matumizi ya mmea huu jinsi inavyofanywa kwa tumbaku na pombe,” Okoth akasema katika barua yake.

Mbunge huyo pia alitaka utafiti ufanywe kuhusiana na matumizi ya bangi katika nyanja ya matibabu, viwandani na katika shughuli za utengenezaji wa nguo na bidhaa za burudani huku akiitaka serikali kuanzisha ushuru kwa sekta ya bangi.

Lakini wakizungumzia suala hilo, kiongozi wa wengi Aden Duale na mwenzake wa mrengo wa wachache John Mbadi walipinga vikali pendekezo la Bw Okoth wakisema kuwa “halina mashiko”.

“Mwenzetu Bw Okoth amepotoka. Bangi ni dawa ya kulevya ambayo imeathiri maisha ya watu wengi nchini, haswa vijana. Spika hafai kuidhinisha pendekezo kama hili,” akasema.

Naye Bw Mbadi akasema: “Namhimiza mwenzangu kuondoa pendekezo hili kwamba chama cha ODM kilichomdhamini bungeni hakiungi mkono matumizi ya dawa za kulevya”.

Na mwanzoni mwa 2018, Bw Sammy Gwada Ogot aliwasilisha ombi katika seneti akitaka bangi ihalalishwe kwa misingi hiyo ya kuwa na uwezo wa kutibu magonjwa.

Hata hivyo, ombi lake liliibua mgawanyiko miongoni mwa maseneta baadhi yao wakitaka ombi lake kutupiliwe mbali huku wengine wakiomba lijadiliwe kwa kina.

“Hatuwezi kupoteza muda na rasilimali za bunge hilo kujadili kitu ambacho kimekuwa kikivuruga maisha ya vijana wetu. ,” akasema Seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri, aliyeunga mkono na mwenzake wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Hata hivyo, maseneta Ladema Ole Kina (Narok), Stewart Madzayo (Kwale), George Khaniri (Vihiga) na Fred Outa (Kisumu) walitaka seneti ialike wataalamu ili watoe ufafanuzi kuhusu madai ya Bw Ogot.

Bw Ogot alidai kuwa taifa hili linaweza kupata Sh1.5 trilioni kila mwaka kutokana na mauzo ya bangi ikiwa pendekezo lake litakubaliwa na kutekelezwa.