Kampuni za viatu zinadorora ila vijana hawa wamejihani na cherehani kuendeleza ushonaji
NA PATRICK KILAVUKA
Ni mafundi vya viatu ambao wanasanii na kusanifu viatu kwa ujuzi wao kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Wanatumia ngozi ya thamani kuongezea ubora wa kudumu.
Evans Odhiambo, Jacob Mbunda, Brian Kibe na Stephen Karimi wanasema baada ya kutafuta kazi bila kufanikiwa, waliamua kupata maarifa ya kazi ya mikono ya kuunda viatu kwa ubunifu mwingi almradi wapate riziki.
Ni kwa kutambua palipo nia pana njia, ambapo mafundi hao wa Gibbs Shoes walioanza kama mafundi wa mkono, sasa ni wa kupigwa mfano kwa kutengeneza viatu vya hadhi ya juu.
Licha ya changamoto za uchumi kusababisha baadhi ya kampuni za kuunda viatu zikipunguza shughuli au hata kuwazia kufunga kazi kutokana na gharama ya juu, vijana wa Gibbs Shoes wamejifunga kibwebwe kuhakikisha wanaunda viatu vya thamani kwa bei nafuu.
Ni matumaini yao kwamba wataweza kushikwa mkono kuinua kazi hii ili vijana wengi wapate maarifa ya kujikimu kimaisha.
Wanasanifu muundo wa viatu kwa weledi hadi kiatu kinamalizika.
Evans Odhiambo na Jacob Mbunda ni mafundi wa cherehani ilhali Brian Kibe na Stephen Karimi wanafanya ya kuunga kiatu, kupiga msasa na kumalizia kiatu.
Wanahakikisha kila nambari ya kiatu imechongeka na iko shwari kwa kutumia mbao ya kila namba kuanzia ya wadogo hadi wakubwa kulainisha na kukisimamisha imara.
Wakitumikia malighafi kama mbao ya kila namba, ngozi ya hadhi ya juu, gundi, nyuzi na kadhalika, aina ya viatu ambavyo wanatengeneza ni vya ‘Amocane’, ‘Loafers’, ‘Sharp Shooters’, ‘Comforts’ na ‘Back to School’.
Aidha, vyaweza kuwa vya kamba au visivyo na kamba kwa kutegemea chaguo la mteja.
Wateja wao ni wale binafsi na wauzaji wa jumla
Kwa wateja wa jumla, viatu hivi vinapatikana kwa viwango wa watoto nambari 7-10 (Sh550) ilhali 10-13 (Sh650) mbali na watoto wakubwa kiasi ambao huvaa 1-4 (Sh700) na kuanzia namba tano huwa Sh900 bei ya jumla.
Kulingana na uwezo, wanasema wanaweza kuunda viatu 20-50 kila siku kwa kutegemea miundo na kazi ya kila kiatu.
Wanasema mtandao wa jamii pia umewasaidia kunadi kazi zao na hata wengi hupiga oda kupitia WhatsApp na kusambaziwa kazi zao kama zimekwisha kukamilika.
Kulingana na mafundi hawa, mtaji wa kuanzisha kazi hii ni angalau Sh50,000.
Cha mno ni mbao za namba tofuati ambapo kila moja hupatikana kwa Sh1,200 na cherehani kwani hivyo ndiyo vyenye changamoto kwa kuanzisha kutokana na gharama ya juu. Hivi vingine vinaweza kupatikana hatua kwa hatua ukiendelea.
Hata hivyo, wanakiri kwamba kazi hii licha ya kuwa inafanywa kwa mikono inakubidi uwe angalau na masomo kiasi kwani inahitaji ujue hisabati pamoja na sayansi kiasi kwani kuna kutumia gundi na unafaa kuwa mwangalifu ili isilete madhara.
Wanakiri kwamba kazi hii ndio imekuwa chanzo cha riziki yao kwa miaka miwili hadi mitano kila mmoja ameifanya kwani imewawezesha kujiajiri, kujitegemea, kutunza jamii, kupata maarifa na ujuzi wa kuunda miundo msingi ya viatu pamoja kutambuliwa kwenye soko la viatu ambalo lina ushindani si haba.