Akili Mali

Ukaushaji mboga za kienyeji wamtekea masoko ng’ambo


UONGEZAJI mazao ya kilimo – shambani thamani ni mojawapo ya mitandao ambayo ikizamiwa pakubwa itasaidia kuangazia kero ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.

Kilimo ni sekta pana na yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi (GDP), hivyo basi kusindika mazao kutafungua mianya zaidi.

Kwa wanaoshiriki, wanakiri tija zake ikizingatiwa ni mtandao unaochangia ukuaji wa sekta ya viwanda.

Nzivoo Katoo, mwanzilishi wa Green Leaf Veggies, yuko kwenye safari kuonyesha tija za mboga asilia za Afrika zilizokaushwa kama nguzo muhimu kuangazia suala la virutubisho na kilimo endelevu.

Analima mseto wa mboga kuanzia kunde, mnavu maarufu kama managu au sucha na mchicha, ndio terere.

Hadithi yake ni ya ubunifu na kujituma kuboresha maisha ya jamii eneo la Ukambani.

Anakumbuka miaka 20 iliyopita, akiongozwa na matamanio ya kuhifadhi mboga yaliyochochewa na wingi wa kunde msimu wa mvua na uhaba wakati wa ukame, Nzivoo alianza kutafiti mbinu faafu kuzihifadhi.

Nzivoo Katoo, mwasisi Green Leaf Veggies akionyesha mboga alizokausha wakati wa Maonyesho ya Sankalp Barani Afrika 2024 jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni kupitia hatua hiyo mbegu ya Green Leaf Veggies ilipandwa na kumea.

Mwaka 2021, katikati mwa changamoto zilizoletwa na janga la Covid-19, Nzivoo aligeuza biashara ya kifamilia kuwa kampuni inayoleta faida.

Alianza na kunde, na muda ulivyosonga akajumuisha managu na terere.

Mjasirimali anasema chocheo kubwa kukausha mboga lilitokana na kuona jinsi wakulima hupoteza mazao msimu wa mavuno hasa wanapokosa soko.

“Wakati wa mavuno, wakulima wengi haswa wasio na miundomsingi kuhifadhi chakula hupoteza mazao wanapokosa wanunuzi,” Nzivoo anasema.

Unapozuru masoko mengi nchini, hutakosa kuona mazao mabichi yaliyotupwa kwenye majaa – yameoza na mengine yakiwa katika hali nzuri.

Hilo si tofauti na yanayoshuhuduiwa shambani, hasa kwa wakulima wa mboga, viungo vya mapishi kama vile nyanya, vitunguu, na vinginevyo, na matunda, taswira inayokwaza mfanyabiashara huyu mchanga.

Mboga aina ya kunde zilizokaushwa na Nzivoo Katoo kupitia kampuni yake ya Green Leaf Veggies. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na takwimu za Wizara ya Kilimo, wakulima nchini kwa mwaka hupoteza kati ya asilimia 20 hadi 40 ya mazao msimu wa mavuno.

Gavana wa Nyandarua, Dkt Kiarie Badilisha kwa mfano anasikitika kwamba kaunti yake hupoteza karibu asilimia 40.

“Kupoteza asilimia 40 ya mazao ya shambani ni kiwango kikubwa mno, ikizingatiwa kuwa kuna maeneo kama vile ya jangwa na nusu jangwa (Asal) ambayo yanaendelea kukosa chakula,” anasema Dkt Badilisha.

Mkondo aliokumbatia kijana Nzivoo, anasema mchango wake ni mdogo sana.

“Ninakadiria mchango wangu wa kuongeza mboga thamani kwa kuzikausha unawakilisha asilimia moja pekee kuokoa mazao msimu wa mavuno,” akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano.

Green Leaf Veggies inahudumu na zaidi ya wakulima 20, 000.

Kulingana na Nzivoo, ameweka viwango vya ubora wa mboga ambavyo wakulima wanapaswa kuafikia, zinakaushwa, na kuhakikisha zinadumisha uhalisia wa virutubisho na ladha.

Afisa Mkuu Mtendaji Green Leaf Veggies, Nzivoo Katoo, akipanga mboga alizoongeza thamani kwa kukausha, wakati wa Maonyesho ya Sankalp Barani Afrika 2024 jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, ana mipango ya mafunzo kuelemisha wakulima mbinu za kuendeleza kilimo bora.

“Mboga tunazochukua, hazipaswi kupitisha siku tatu baada ya kuvunwa,” akaarifu mwekezaji huyu.

Anatumia mifumo asilia ya kawi – jua kukausha mboga, na anaomba kupigwa jeki kuwekeza katika mitambo ya kisasa na kiotomatiki ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.

Kwa sasa, anakausha tani 2.5 kila baada ya siku mbili, kipimo cha gramu 50 akiuza kuanzia Sh100 na gramu 80 Sh200 kulingana na aina ya mboga.

Kwa ajili ya ubora wa mboga alizokausha, Nzivoo anafichua kwamba amepenyeza soko hadi ng’ambo kwa mataifa kama Uhispania, Bahrain, Milki za Kiarabu (UAE), na Amerika, Barani Afrika, Ghana ikiwa mteja wake.

“Nimevumisha Green Leaf Veggies kupitia mitandao ya kijamii, na wengi ni wateja wanaozuru Kenya na kununua bidhaa wakirejea kwao,” anaelezea.

Nzivoo Katoo, mwanzilishi Green Leaf Veggies ana mchango mkubwa katika sekta ya mboga kufuatia jitihada zake kuziongeza thamani kwa kuzikausha. PICHA|SAMMY WAWERU

Akiwa na Shahada ya Hesabu na Masuala ya Kompyuta na Sayansi, Nzivoo ana imani njia aliyochukua siku moja itazaa matunda matamu.

Anasisitiza haja na umuhimu wa kuongeza bidhaa za kilimo thamani ili kuteka soko lenye ushindani mkuu.

Kutokana na jitihada zake, alikuwa miongoni mwa wajasirimali waliopata fursa kushiriki Maonyesho ya Sankalp Barani Afrika 2024, makala ya 11 yaliyofanyika kati ya Februari 28 na 29.

Aidha, alishiriki kupitia ufadhili wa Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) na Scaling Up Nutrition Business Network (SBN).

Kauli mbiu ya maonyesho hayo yaliyofanyika jijini Nairobi ilikuwa ‘Kupiga jeki Ujasirimali Barani Afrika ili Kuwahi Maendeleo ya Kimataifa’.