Akili MaliMakala

Kutana na Shosh anayeunda yoghurt

Na NA SAMMY WAWERU June 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MARGARET Ruguru ni kati ya wafugaji mashuhuri wa ng’ombe wa maziwa nchini na endapo kuna hatua anayojivunia ni kukumbatia mfumo wa uongezaji thamani.

Mkulima huyu ambaye unapotangamana naye hujitambua kama ‘Shosh’, amekuwa kwenye ufugaji kwa zaidi ya miaka 20.

Kulingana na Margaret, alipoingilia ufugajibiashara huo mwaka 2000, anasema soko lilikuwa bora kwa sababu alikuwa ameajiriwa katika mojawapo ya chama cha ushirika cha maziwa Murang’a.

Hivyo basi, alikuwa na mianya ya soko la bidhaa aliyozalisha.

“Nilianza na ng’ombe mmoja, na niliendelea kuongeza muda ulivyosonga,” Margaret anasema.

Mume wa Margaret Ruguru kwenye zizi la ng’ombe wanaofuga Murang’a. PICHA|SAMMY WAWERU

Ufugaji anaoendeleza aliuingilia kama mbinu ya kujipa mapato ya ziada, na mahesabu yake yaliingiana.

Hata hivyo, 2007 alipofutwa kazi mambo yalienda mrama Margaret akikadiria hasara bin hasara aliyoshuhudia.

Anafanya ufugaji eneo la Gatanga, Kaunti ya Murang’a, na kilomita chache kutoka Mji wa Thika.

Anakumbuka akichuuza maziwa vijijini na hata Thika, baada ya hoteli aliyokuwa akiisambazia kusimamisha ghafla kandarasi.

“Usimamizi ulidai walikuwa na ng’ombe kadhaa ambao walizaa, hivyo basi tatizo la maziwa liliwaondokea,” anaelezea.

Huo ukawa mwanzo wa kuchukua dira nyingine kutafutia bidhaa yake soko.

Mama huyu mkakamavu anakumbuka akihangaika kuchuuza lita 200 za maziwa.

Margaret Ruguru, akielezea kuhusu maziwa ya mtindi anayounda, akiwa kwenye kiwanda chake Gatanga, Murang’a. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni kiwango kikubwa ambacho kwa mkulima kukosa soko ni hasara isiyomithilika.

Simulizi za wafugaji kumwaga maziwa na mengine kuyapa wanyama wa nyumbani, Margaret anaelewa bayana.

Ni katika pilkapilka za mahangaiko alielekezwa kwa Idara ya Ufugaji Kaunti ya Murang’a, ambayo ilimfumbua macho.

Idara hiyo iliniunganisha na Shamba la Maonyesho la Mariira, Murang’a ambalo hutoa mafunzo ya ufugaji bora na kwa utalaamu, pamoja na uongezaji mazao – maziwa thamani, anadokeza.

Huo ulikuwa mwaka wa 2016.

“Kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta(JKUAT), nilinolewa makali jinsi ya kuunda maziwa ya mtindi (maarufu kama yoghurt),” Margaret akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano ya kipekee.

Mama huyu na bwanake, vilevile, walifunzwa jinsi ya kupunguza gharama ya ufugaji kwa kujiundia malisho.

Margaret Ruguru (kulia) na mmoja wa maafisa kutoka Idara ya Kilimo na Ufugaji Murang’a (kushoto) aliyemuonyesha mbunu za uongezaji maziwa thamani, kwenye maonyesho ya bidhaa za kilimo Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Alifichua kwamba mafunzo hayo aliyapokea kupitia kwenye kundi la wafugaji wapatao 50.

Aidha, ilimgharimu Sh5, 000 kupata mafunzo hayo.

Miradi ya serikali kupiga jeki sekta ya kilimo na ufugaji, wakulima wanashauriwa kuwa kwenye makundi au vyama vya ushirika ili kunufaika.

Mafunzo ya uundaji maziwa ya mtindi, Margaret anasema yalifungua chapta mpya katika biashara yake kukwepa hasara ya mara kwa mara.

Kwa ushirikiano na mume wake, wanamiliki kiwanda cha kutengeneza yoghurt kinachojulikana kama Sky Blue Farmlands.

Aidha, kina mashine ya kuchemsha maziwa (pasteurizer), kuyapoesha (cooler) na kuyapakia (yoghurt sealing).


Margaret Ruguru hutengeneza brandi ya yoghurt aina ya Strawberry na Vanilla. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni biashara anayoiendelezea kwenye kipande cha shamba chenye ukubwa wa futi 100 kwa 80, ambacho pia kinajumuisha mradi wa ng’ombe, kuku wa kienyeji walioimarishwa, samaki na upanzi wa malisho.

Hutengeneza brandi ya Strawberry na Vanilla, shabaha ikiwa vinywaji vyenye virutubisho faafu mwilini – probiotic.

Soko hulenga wanunuzi wa jumla kama vile supamaketi na maduka makuu ya bidhaa za kula na kunywa.

Hutumia majukwaa kama vile maonyesho ya kilimo na ufugaji kunogesha bidhaa zake.