Habari za Kitaifa

Maandamano yashika kasi jijini


MAANDAMANO kupinga mswada wa Fedha yameshika kasi j katikati mwa jiji la Nairobi huku biashara zikisalia kufungwa.

Mamia ya waandamanaji, wengi wao wakiwa ni vijana wanaimba nyimbo za kukosoa Rais William Ruto na serikali yake kwa kuwatelekeza vijana kinyume na alivyoahidi katika kampeni zake na manifesto ya Kenya Kwanza.

Katika barabara ya Moi, makundi ya vijana walishirikisha maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia katika mchezo wa paka na panya.

Kila wakati wakiona gari la polisi, wanapiga mbinja, kupuliza firimbi na vuvuzela.

Polisi wakiwa juu ya magari ya Land Cruiser wanafyatua mikebe ya kutoza machozi kuwatawanya waandamanaji.

Hata hivyo, bila kujali moshi wa vitoza machoji waandamanaji wanakusanyika tena katika makutano ya barabara ya Kimathi na Kenyatta wakiimba nyimbo.

Waandamanaji hawarushi mawe, hawafungi barabara na hawatatizi magari.

“Hatuna haja ya kurushia yeyote mawe, hatufungii magari kupita ila letu ni kupaaza sauti rais na serikali yake wajue wanakadamiza Wakenya na vijana walipewa ahadi ghushi. Maisha ni magumu,” msichana wa umri wa miaka 23 kutoka chuo kimoja jijini aliambia Taifa Dijitali.