Mswada tata wa Fedha wapita hatua ya pili licha ya maandamano
WABUNGE wamepitisha Mswada wa Fedha 2024 licha ya pingamizi nyingi kutoka kwa umma.
Baada ya upigaji kura uliofanyika Alhamisi alasiri, wabunge 204 walipiga kura ya ‘Ndio’ huku 115 wakipiga kura ya ‘La’.
Hii inamaanisha kwamba mswada huo umepita hatua ya pili na unaingia hatua ya tatu ambapo ukipita pia katika hatua hiyo, utakuwa sheria.
Haya yanajiri katika siku iliyoshuhudia maandamano makubwa kutoka kwa vijana katika maeneo mengi nchini, wakilalamikia kwamba baadhi ya mapendekezo yaliyo kwenye mswada huo yanawakandamiza kiuchumi.
Waandamanaji ambao wengi wao ni chipukizi almaarufu Gen Z wanasema vipengele vinavyolenga kuongeza ushuru vitafanya maisha yawe magumu zaidi, wakati ambapo wananchi wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya uchumi.
Awali, akizungumza mjini Garissa baada ya kuhudhuria sherehe ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Garissa, Rais William Ruto aliwataka wabunge kupitisha mswada huo, akisema utasaidia kuendeleza miradi muhimu ikiwemo mpango wa lishe shuleni pamoja na mikopo ya elimu ya juu, almaarufu Helb.
Sasa mswada huo unaenda kwenye hatua ifahamikayo kama “Committee Stage” ambapo mapendekezo yakiwemo yale yaliyotangazwa na wabunge wa UDA Jumanne baada ya kukutana na Rais, ya kufuta ushuru wa mkate, magari, kutuma pesa kwa simu, mafuta ya kupikia, yatajadiliwa na ama kujumuishwa, au kukataliwa kabla sasa mswada huo usomwe kwa mara ya mwisho katika hatua ya tatu.