Dimba

Yafichuka kumbe majambazi waliiba Kombe La EPL ambalo Man City walishinda

Na CHRIS ADUNGO June 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NUSU ya Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lilibadilishwa kisiri baada ya kuibwa, gazeti la The Sun limefichua.

Wezi nchini Ubelgiji walivamia sanduku lilimokuwa kombe hilo wakaiba sehemu ya juu (kichwa) na chini (kitako) zinazokadiriwa kuwa za thamani ya Sh41 milioni. Wizi huo ulifanyika mwishoni mwa 2022.

Ingawa usimamizi wa EPL ulifanikiwa kuficha chini ya maji tukio hilo la wizi, sehemu zilizoibwa za kombe hilo hazijawahi kupatikana.

Ufichuzi huo ulibainishwa kwa umma wiki hii, wakati vinara wa EPL walitangaza ratiba ya msimu mpya wa 2024/25.

Wakuu wa EPL hawakutaka kutangaza kwamba kichwa na kitako – chenye uzani wa kilo 15.9 – ziliibwa katika hafla ya kampuni moja nchini Ubelgiji.

Iliaminika kuwa wezi hao hawakujua kilichokuwa ndani ya sanduku husika, na inawezekana sehemu walizonyofoa tayari zimeyeyushwa.

Kwa kawaidia EPL huwa na makombe mawili yanayofanana, kila moja likiwa limewekewa bima ya Sh82 milioni.

Kombe moja linahifadhiwa na mabingwa huku lingine likisalia na vinara wa EPL — ndilo ambalo huzungushwa kote ulimwenguni kwa mashabiki kutazama.

Mara nyingi, kombe hilo hutengewa kiti chake ndani ya ndege na hulindwa sana na maafisa wa usalama kwenye hafla yoyote.

Kampuni ya Asprey London ambayo hutengeneza makombe hayo iliombwa kuunda kombe jingine sawa na lile ambalo mabingwa walikuwa wametuzwa, baada ya wizi huo uliofanyika Ubelgiji mwishoni mwa 2022.

Mnamo 1966, miezi minne kabla ya Kombe la Dunia kuanza nchini Uingereza, kombe la Jules Rimet liliibiwa huko jijini London.

Wiki moja baadaye, David Corbett alikuwa akitembea na mbwa wake Pickles walipolipata kwenye vichaka huko Upper Norwood, London Kusini.

Corbett alituzwa Sh820,000 huku jibwa lake, Pickles, likipokezwa medali.

Usimamizi wa EPL unatazamiwa kutoa maoni wakati wowote wiki ijayo.