Habari za Kitaifa

Dalili ya uwezekano wa ndoa ya kisiasa kati ya Gachagua na Kalonzo kuelekea 2027

Na MWANGI MUIRURI June 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DALILI kwamba ndoa mpya ya kisiasa inasukwa kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka zilijitokeza Ijumaa baada ya wawili hao kushiriki jukwaa moja hadharani katika Kaunti ya Kiambu.

Bw Musyoka, ambaye alikuwa ameandamana na kiongozi wa chama cha DAP-Kenya Eugene Wamalwa, alimhakikisha Gachagua kwamba Azimio itapinga jaribio la kumng’oa mamlakani.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kuwa, “hii ni mara yangu ya kwanza kuketi kando ya Naibu Rais na ninakiri kwamba nimefurahishwa na bidii yake ya kutetea misimamo yake.”

“Kwa hivyo nataka kuwaambia wale wabunge wasio na heshima kwamba wakijaribu kuleta hoja ya kumwondoa afisini Gachagua uongozi wa Azimio na wanachama wake wataiangusha,” Bw Musyoka akasema.

Alieleza kuwa hoja ya kipekee ambayo wabunge wa upinzani wataunga mkono ni ile ambayo inalenga kuwaondoa Rais William Ruto na Bw Gachagua kwa pamoja.

Kauli ya Bw Musyoka iliwashangaza wengi ikizingatiwa kuwa rais wa zamani Uhuru Kenyatta, kimsingi, ni mwanachama na mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio.

Bw Kenyatta alimuunga mkono kiongozi wa Azimio Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 lakini akashindwa kwa kura chache na Rais William Ruto.

Uhasama kati ya Gachagua na Bw Kenyatta

Bw Gachagua amekuwa akijitahidi kumaliza uhasama kati yake na Bw Kenyatta kiasi cha kumuomba msamaha hadharani kwa kumshambulia kwa maneno makali, pamoja na watu wa familia yake, wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Musyoka anaonekana kumkaribia Bw Gachagua, kisiasa, wiki mbili baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuunga mkono pendekezo kwamba mapato ya kitaifa yanapasa kugawanywa kwa misingi ya wingi wa watu.

Hatua ya Odinga kuunga mkono mfumo huo, maarufu kama “mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja” iliibua uvumi kuhusu kuwepo kwa ukuruba wa kisiasa kati ya Mlima Kenya na Azimio.

Uamuzi wa Bw Gachagua kupigia debe mfumo huo wa ugavi wa mapato umekosanisha na wandani wa karibu wa Rais Ruto wakiongozwa na Waziri wa Usalama Kithure Kindiki na mshauri wake wa masuala ya kiuchumi David Ndii wanaoupinga.

Bw Musyoka pia amemminia sifa Bw Gachagua miezi miwili baada ya kukutana na baadhi ya wanachama wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu wakiongozwa na mwenyekiti wao Wachira Kiago.

Wakati wa mkutano huo walitoa taarifa ya pamoja wakisema kuwa wanapania kubuni muungano wenye manufaa kwa jamii za Wakikuyu na Wakamba

Baada ya mkutano huo wa Aprili 4, 2024 katika Kaunti ya Kiambu, Bw Musyoka alidai yeye ndiye daraja la kihistoria kati ya jamii za Agikuyu na Akamba ambazo ni mashemeji.

Naye Mzee Kiago alisema hivi: “Ushirikiano kati yetu utaimarika zaidi na kuleta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”

Mnamo Ijumaa, akiongea katika hafla ya kutawazwa kwa Askofu wa Kanisa la African Independent Pentecostal Churches of Africa (AIPCA) Benson Gathungu, Bw Musyoka alimwambia Gachagua hivi: “Hatutachoka kukuunga mkono. Hata kama wapinzani wako wanakusukuma zaidi jisikie huru kukimbilia nyumbani Mlima Kenya na tutakusaidia,”akasema.

Kando na Gachagua, wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Bw Wamalwa, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Senata wa Kiambu Karungo Thang’wa, Mbunge wa Ruiru Simon King’ara, magavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu na James Nyoro na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Catherine Waruguru.