Makala

TUONGEE KIUME: Kukosa nguvu za kiume ni msingi tosha wa talaka mahakamani

Na BENSON MATHEKA June 23rd, 2024 2 min read

MKEO akigundua kwamba hauwezi kumtimizia haki yake ya tendo la ndoa na kwamba ulimficha kabla ya kuoana kwamba hauna nguvu za kiume, anaweza kukutaliki.

Hii mojawapo ya sababu zinazotambuliwa kama misingi ya talaka kortini. Ni muhimu kufahamu kuwa talaka inatambuliwa kisheria kupitia sheria ya ndoa ya Kenya na kabla ya kuanza mchakato wa talaka, ni lazima mtu awe na sababu za kutosha, ikiwemo kutambua kwamba mumewe hana nguvu za kiume na hakuwa akifahamu hayo kabla ya kuoana rasmi.

Vile vile, mtu akigungua mume au mke anaugua ugonjwa wa zinaa usioweza kutibika na unaoweza kuambukizwa, ana haki ya kuomba talaka mradi tu athibitishie mahakama kwamba hakuwa na habari mwenzake alikuwa akiugua kabla ya kuoana.

Ni muhimu kufahamu kuwa ndoa haiwezi kuwa ndoa iwapo hatatiwa muhuri kwa wachumba kushiriki tendo la ndoa.

Sababu nyingine ya talaka kukubaliwa na iwapo mmoja wa wachumba anashiriki mipango ya kando. Kufanya tendo la ndoa na mtu mwingine kando na mume au mkeo ni kigezo cha talaka. Talaka nyingi nchini Kenya huwa zinazotokana na uzinifu, maarufu kama mipango ya kando nilivyotaja hapo juu. Hata hivyo, ni lazima anayewasilisha kesi ya talaka aweze kuthibitisha madai yake mbele ya korti.

Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, talaka inaweza kupeanwa kutokana na ukatili wa mtu kwa mume au mkewe.

Ukatili huu, unaweza kuwa wa kimwili au kiakili au unyanyasaji unaoweza kuthibitishwa kortini. Hivyo, ni muhimu kuepuka tabia inayoweza kuhatarisha maslahi ya mumeo au mkeo ili kuepuka talaka.

Watu wanaowakwepa wachumba wao bila sababu maalum kwa miaka mitatu huwa wanaalika talaka. Sheria ya ndoa ya Kenya inasema mtu anayeachwa kwa kipindi hicho na mume au mkewe anaweza kuwasilisha kesi ya talaka. Hii sawa na wachumba kutengana kwa muda wa zaidi ya miaka minne.

Ili kigezo hiki kiweze kutumiwa kutoa cheti cha talaka, ni lazima mlalamishi athibitishe kuwa ametengana na mume au mkewe kwa miaka minneĀ  na zaidi huku kila mmoja wao akiishi kivyake.

Vile vile, ni lazima kutengana kwao kuwa kwa hiari na wachumba wote wawili wakubaliane kuwa ndoa yao imevunjika kiasi cha kutorekebika.

Kigezo kingine cha talaka ni mume au mke kupatwa na matatizo ya akili yasiyoweza kutibika.

Hali hii ni lazima ithibitishwe na madaktari wawili na mume au mke awe ameugua kwa miaka minne.