Oguda, wengine saba wakamatwa alfajiri maandamano yakiwadia
MCHAMBUZI wa siasa na mwanaharakati wa mitandao ya kijamii Gabriel Oguda ni miongoni mwa watu 9 waliodaiwa kukamatwa alfajiri Jumanne, Juni 25, saa kadha kabla ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Wengine waliodai walivamiwa na maafisa wa usalama nyumbani Osama Otero ambaye amekuwa akiandaa vikao katika X spaces zinazopinga Mswada wa Fedha wa 2024. Osama Otero aliripotiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana.
Watumiaji wengine wa X ambao wanashukiwa kutekwa ni pamoja na; Drey Mwangi, TemperCR7, Harriet, Shad, Franje, Worldsmith na Hilla254.
Katika ujumbe wake wa mwisho kabla ya kwenda ya kutoweka katika mtandao, Gabriel Oguda alisema kuwa polisi walikuwa katika mlango wa nyumba yake. Kulikuwa na wasiwasi kwamba watekaji wake walikuwa wakitumia simu yake kwa kuwa akaunti yake X iliendelea kutuma wito wa kuwataka Wakenya kujitokeza kwa maandamano.
Katika kile kilichoonekana kuwa operesheni iliyoratibiwa, Osama Otero, aliandika katika X kuhusu watu asiowafahamu nyumbani kwake wakati sawa na Oguda.
“Kuna watu nje ya nilipo,” alisema katika chapisho lake la mwisho ambalo lilisambazwa kwa kasi huku hashitegi #FreeOguda na #FreeOsama zikiundwa na kutawala X muda mfupi baada ya kutekwa nyara.
Hashitegi #RejectFinanceBill2024 sasa imesambaa duniani kote ikiwa imechapishwa mara milioni 3.59 kufikia Jumanne asubuhi na kuifanya kuwa mada inayovuma zaidi Afrika Mashariki.