Habari za Kitaifa

Wandayi: Yuko wapi Gabriel Oguda?

Na CHARLES WASONGA June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wachache Opiyo Wandayi amelalamika kwamba mfanyakazi katika afisi yake Gabriel Oguda alikamatwa usiku wa kuamkia Jumanne, Juni 25, 2024 bila sababu maalum.

Akiongea bungeni Jumanne asubuhi aliposimama kwa hoja ya nidhamu, Bw Wandayi alitaja tukio hilo kama kuingiliwa kwa uhuru wa Bunge kwani ulitokea wakati ambapo wabunge wanashughulikia Mswada wa Fedha wa 2024 katika awamu ya tatu.

Mswada huo tata, hata hivyo, ulipitishwa na unasubiri Rais William Ruto kuutia saini kuwa sheria.

Mbunge huyo wa Ugunja alifichua kuwa Oguda alimpigia simu mwendo wa nane za usiku wa kuamkia Jumanne akijulisha kuwa watu aliowataja kama maafisa wa polisi walivamia makazi yake.

“Muda mfupi baadaye, simu yake ilizongwa na singeweza kumfikia hadi saa kumi na mbili na nusu asubuhi,” Bw Wandayi akasema.

“Baadaye niliwaita kundi la mawakili kuingilia kati masaibu yake lakini mpaka sasa hawajampata katika kituo chochote cha polisi Nairobi. Bw Spika hatuwezi kuruhusu vitendo kama hivyo vya maafisa wa polisi kutumiwa kuwateka nyara Wakenya bila sababu yoyote na kuwafungia,” Bw Wandayi akaeleza.

“Sasa Bw Spika hatujui ikiwa watu waliomteka afisa huyo anayehudumu katika afisi yangu walimuua au la,” akaongeza.

Kwa upande wake kiongozi wa wengi Kimani Ichungw’ah aliahidi kumpigia simu Inspekta Jenerali wa Polisi, IG, Japhet Koome kumuuliza kuhusu tukio la kukamatwa kwa Bw Oguda.

“Nitamfikia Koome kubaini ikiwa ni kweli maafisa wa polisi ndio walimkata Oguda au la. Na endapo ni kweli alikamatwa kwa kosa fulani, awasilishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria,” akasema.

“Hili ni suala lenye uzito mkubwa zaidi. Leo ni afisa aneyehudumu katika afisi ya Wandayi ambaye amekamatwa, kesho ni afisa katika afisini ya Kagombe (Gabriel Kagombe, Mbunge wa Gatundu Kusini) na Kimani Ichung’wah (yeye) atakamatwa. Sharti usalama wa maafisa wanaowahudumia wabunge upewe kipaumbele,” Bw Ichungwa’h akaeleza.

Spika Moses Wetang’ula pia aliamuru kwamba afisi ya kiongozi wa wengi ifuatilie kubaini ukweli kuhusu kukamatwa kwa Bw Oguda.

Kando na kuwa mfanyakazi katika afisi ya Bw Wandayi, Bw Oguda pia ni mtumizi wa mitandao ya kijamii mwenye ufuasi mkubwa (influencer) na mchangiaji katika safu ya maoni, gazeti la “Saturday Nation”.