Habari za Kitaifa

Ni kweli intaneti ‘imenyongwa’, shirika la uangalizi lasema huku maandamano yakichacha

Na CECIL ODONGO, DANIEL OGETTA June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

LICHA ya serikali kuwahakikishia Wakenya kuwa intaneti haingevurugwa, Wakenya mnamo Jumanne walitatizika mitandaoni kutokana na kasi ya chini ya  intaneti.

Haya yalifanyika wakati maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 20244 yalishuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini. Vifo  viliripotiwa huku uharibifu wa mali pia ukitokea katika miji ambayo maandamano yalifanyika.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CAK) David Mugonyi mnamo Jumatatu alikuwa amepuuza madai kuwa serikali ilikuwa ikipanga kuzima intaneti.

Lakini shirika la uangalizi la masuala ya intaneti, International internet observatory Netblocks kupitia kwa chapisho lake kwenye mtandao wa X Jumanne jioni lilithibitisha kuweko kwa “uvurugwaji mkubwa wa intaneti nchini Kenya”.

Awali Jumatatu, madai yalizuka kuwa mpango wa kuzima intaneti ulikuwa mbinu ya serikali ya kukabili wingu la maasi na maandamano yaliyoandaliwa na vijana kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Bw Mugonyi alisema CAK ilikuwa imepokea maswali iwapo intaneti ingezimwa. Hata hivyo, alihakikishia Wakenya kuwa serikali haikuwa na mpango huo.

“CAK haina nia ya kuzima intaneti,” akasema Bw Mugonyi akiongeza kuwa hatua hiyo inaenda kinyume cha Katiba na uhuru wa kujieleza.

Katika taarifa ya pamoja, Shirika la Kimataifa la Amnesty Kenya, washirika wake na mashirika ya kijamii, yalikuwa yamedai kuwa serikali ya Rais William Ruto ilikuwa ikipanga kuzima intaneti.

Amnesty Kenya ilikumbusha serikali kuwa kuzima Intaneti au kuivruga, kupiga marufuku heshitegi nyingi dhidi ya Mswada wa Fedha 2024  au matukio kupeperushwa mbashara, ni kuvunja haki za kibinadamu za raia.

Maandamano yalipochacha, Wakenya watumiaji wa mitandaoni walifikiwa huku malalamishi ya intaneti ya kasi ya chini yakitanda.

Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, Wakenya walionyesha kero zao kuhusu kasi ya intaneti ambayo ilikuwa chini na kuwazuia kufuatilia matukio. Wakenya wamekuwa wakitumia intaneti kuvumisha pingamizi zao dhidi ya Mswada wa Fedha 2024 ambao ulipitishwa jana na wabunge.

Kupitia X (zamani Twitter), Wakenya ambao walikuwa wakipeperusha matukio mbashara, walilalamikia kutatizwa na intaneti.

“Safaricom wamefinya intaneti bana. Kwangu X inaenda polepole, Nyie watu mmeathirika?” akalalamika Muhammad Onyango.

Mwengine Edgar Wabwire aliandika “Intaneti imeingiliwa na kudhibitiwa watumiaji wakianza kutatizika kutokana na kasi ya chini.”