Habari za Kitaifa

Wahariri wa mashirika makuu walivyombana Rais na maswali mazito kuhusu maandamano

Na BENSON MATHEKA July 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WAHARIRI wa mashirika makuu matatu ya habari nchini walimbana Rais William Ruto na maswali mazito kwa masaa mawili wakati wa mahojiano jana Jumapili katika Ikulu ya Nairobi.

Mahojiano hayo yalijiri siku chache baada ya kisa kilichotikisa nchi Jumanne iliyotangulia, ambapo maandamano kuhusu Mswada wa Fedha 2024 yaliishia kwa Majengo ya Bunge kuvamiwa na sehemu kuchomwa, mauaji, uporaji na uharibifu mkubwa wa mali kufanyika.

Mahojiano hayo ambayo yalikita katika maudhui kama mauaji ya vijana waandamanaji wasio na silaha kupitia kupigwa risasi na polisi, kilio na matakwa ya vijana almaarufu Gen Z, matumizi mabaya ya pesa serikalini, ufisadi, majigambo ya viongozi yalilenga kubaini iwapo Rais Ruto amefahamu bayana wanachokitaka vijana ambao wameandamana kwa wiki mbili sasa.

Rais alijizatiti kujibu makombora ya maswali aliyorushiwa, na kwa kiwango kikubwa ikaeleweka kwamba kuna hatua kali atachukua kwenda mbele, na kwamba Wakenya wanapaswa kumpa muda tu kujionea wenyewe.

Lakini wachanganuzi wa masuala ya kijamii wanasema maandamano ya vijana wa kizazi cha Zoomer, wanaojiita Gen Z, yanapaswa kugutusha serikali na wanasiasa wakome kutumia raia kama vyombo vya kuingia mamlakani na kuwasahau.

Na ili kutuliza hali, serikali inapaswa kubadilisha mikakati yake ya kukabiliana na uasi wa vijana hao ambao ni asilimia 65 ya raia wote wa nchi hii kama vile kuteka nyara wanaoonekana kuwa na ufuasi na usemi mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Vijana hao walitumia tekinolojia kupanga na kuratibu maandamano hayo bila kuegemea misingi ya kikabila au kidini na wadadisi wanasema serikali itakosea kwa kutumia ukabila na dini kuwagawanya, mbinu ambayo inaweza kutumbukiza nchi katika machafuko sawa na yaliyokumba nchi mwaka wa 2008.

Kuzima uasi mkubwa unaonukia ni kuwasikiliza vijana

“Mbinu ya kipekee ambayo serikali inaweza kutumia kuzima uasi mkubwa unaonukia ni kuwasikiliza vijana kwa kupatia kipaumbele maslahi yao ambayo ni upatikanaji wa elimu nafuu na ajira, kuepuka sera zinazowakadamiza na kutumia ujuzi, weledi na nguvu wanazotumia kuzua uasi kujenga nchi yao,” asema mdadisi wa siasa James Kasoa.

Anasema hivi ndivyo vijana hao wanavyoambia serikali kupitia matakwa mapya ambayo wameanza kutoa baada ya rais kukataa kutia saini mswada wa fedha 2024 waliopinga.

Wanachosema vijana hao, aeleza Kasoa, ni uwajibikaji katika serikali. Wanaambia serikali ijirekebishe, ikomeshe ukabila, iwe na uwazi katika shughuli zake, ipunguze matumizi mabaya ya ofisi za umma na ikomeshe ufisadi. Ujumbe wao ni wazi; kwamba wamesubiri serikali itimize ahadi inazotoa kufanikisha maswala haya bila kuona matunda na wamechoka,” aeleza Kasoa.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, mnamo Jumanne, vijana ambao hawakuwa na silaha, kwa maelfu, walivamia majengo ya bunge kuonyesha hasira zao baada ya wabunge kupitisha mswada wa fedha 2024 wakati ambao walikuwa barabarani kuupinga.

“Wabunge walidhani wito wa vijana ulikuwa wingu linalopita. Walichukulia kwamba ilikuwa kawaida na kwamba walikuwa salama ndani ya majengo ya bunge hadi pale vijana walipoyavamia,” akaeleza Kasoa.

Kulingana na Betha Asiko, mchanganuzi wa siasa na mwanauchumi, matakwa mapya ya vijana kwa serikali ya Kenya Kwanza ni ishara kuwa wanataka ibadilishe sera zake ziweze kuwafaa na hii haiwezi kufanyika ikitumia nguvu dhidi ya waandamanaji.

“Kwa sasa serikali imepeleka wanajeshi kukabili waandamanaji jambo ambalo sio ishara nzuri. Kutumia jeshi kuzima uasi wa kiraia ilhali inapaswa kuwa ikilinda nchi dhidi ya maadui kutoka nje ni ishara ya serikali kufeli katika majukumu yake,” asem,a Asiko.

Vijana hao sasa wanataka serikali iheshimu maagizo ya mahakama na kufuta nyadhifa ilizounda kinyume cha sheria kama zile za manaibu wa mawaziri maarufu kama CAS, na kuondoa ufadhili kwa afisi za wake wa rais, naibu rais na mkuu wa mawaziri.

“Na sio kutoa matakwa ya kuondolewa tu kwa ufadhili huo. Wanajua pesa hizo zinaweza kutumiwa kwa shughuli muhimu kwa nchi kama kuajiri walimu na madaktari. Hawa ni watu wanaoambia serikali haifai kuongeza ushuru, inafaa kutumia uliopo vyema,” Asiko asema.

Matakwa mengine ya vijana hao ni kuondolewa kwa ushuru wa nyumba, maelezo ya jinsi pesa hizo zimetumiwa tangu ushuru uanzishwe na waliokatwa warudishiwe makato yao yote.

Vile vile, wanataka maafisa wote wa serikali walio na rekodi za uhalifu na uadilifu wafutwe kazi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iundwe ndani ya siku 30 huku mshahara wa wabunge ukipunguzwa hadi Sh200,000 ili kupata pesa za kuajiri walimu na madaktari.

Kulingana na wadadisi, matakwa haya yote yanaonyesha kwamba serikali imekuwa ikipuuza vijana ambao wanasiasa walitumia wakati wa kampeni.