Ruto akubali kukutana na vijana katika jukwaa la X
RAIS William Ruto sasa amekubali kufanya mazungumzo na vijana wa Gen-Z kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii, haswa X (awali Twitter) ili asikize malalamish yao, moja kwa moja.
Kwenye mahojiano na wahariri wa mashirika makuu ya habari nchini, Jumapili, Juni 30, 2024, Dkt Ruto alieleza kuwa mikutano hiyo itaendeshwa sambamba na ile ya kamati shirikishi aliyobuni kushughulikia matakwa ya vijana hao.
“Ningependa kuwaambia kuwa niko tayari kukutana nao hata katika majukwa ya X. Hii ni licha ya kwamba nimependekeza kubuniwa kwa kamati nyingine ya kuendesha mazungumzo hayo. Sitaki kufungia nje mapendekezo yoyote. Hii ndio maana ninataka kusikiliza kila mtu na kwa njia yoyote ile,” Dkt Ruto akasema.
Rais alisema hayo baada ya wahariri hao, Joe Ageyo (NTV), Eric Latif (KTN, Spice FM) na Linus Kaikai wa runinga ya Citizen kumwarifu kuwa vijana hao wamekataa wazo lake la kubuni kamati ambayo kwayo atakutana nao ana kwa ana asikize malalamishi yao.
Dkt Ruto aliarifiwa kuwa Gen-Z hawana viongozi ambao wanaweza kuwawakilishi katika Kamati hiyo ya wanachama 100.
“Mheshimiwa Rais vijana wa Gen-Z wamekualika kwa mkutano katika jukwaa la X kwa sababu wanasema hawana viongozi watakaowawakilisha katika kamati uliobuni kuendesha mazungumzo kuhusu masuala waliyoibua,” Bw Ageyo akamwambia.
Hata hivyo, Rais alisema kuwa anafahamu matakwa ya vijana hao kwa sababu yeye ana watoto wenye umri kama huo.
“Najua kwamba vijana wetu wanalalamikia masuala kama ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama ya maisha, ufisadi, uwepo wa afisi zisizo na manufaa kwa nchi, mzigo wa madeni, utawala mbaya miongoni mwa masuala mengine. Serikali yangu imeweka mipango kama ujenzi wa nyumba na kuanzishwa kwa vituo vya kidijitali katika maeneobunge yote katika jitihada za kushughulikia changamoto kama hizi,” Dkt Ruto akasema.
Ikiwa Rais Ruto atatimiza ahadi ya kukutana na vijana hao katika jukwaa la X, basi huenda akakumbana na maswali mazito na ambayo yatawasilishwa kwa lugha isiyo ya heshima kama ilivyo ada kwa baadhi ya Gen-Zs hao.