Makala

ADUNGO: Nafasi ya lugha asili katika kusambaza tamaduni

January 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA CHRIS ADUNGO

MATUMIZI ya lugha huwa ndio msingi wa kuendeleza, kukuza, na hata kubuni uzushi mpya katika mirathi ya kitamaduni, mila na hulka za kijamii.

Neno jipya aghalabu huwa ni kizazi cha wazo jipya, na fikira mpya ndiyo huzaa neno jipya.

Si ajabu pia kuwa neno hilo likishakubaliwa na wenye lugha katika kundi fulani la watu, kisha likafikia daraja la kutumika sana, basi vitendo, tabia au mitindo ya wanajamii pia hufuata matumizi ya neno hilo jipya. Kinyume chake pia huenda kikatokeza, yaani mtindo mpya wa jamii kuwa ndiyo mbinu ya kuzuka kwa neno jipya.

Kwa hivyo, si rahisi kwa lugha kutengana na taswira za jamii: utu, utamaduni, mila, mitindo na mengineyo.

Kulingana na uhusiano wa lugha za eneo letu la Afrika, aila nne kuu za lugha zinatambuliwa kuwa ni lugha halisi za Kiafrika: Nilo-Sahara (mfano Kidholuo, Kiyomba); Niget-Kongo (kama lugha za Kibantu); Afrika-Asia (Kiamhara, Kiarabu; Kitigre); Khoisan (Kixhosa).

Kwa kutumia sifa za kilugha basi, lugha yoyote iliyokaa nje ya aila hizi itahesabika kuwa ni lugha isiyo na uhusiano wowote na lugha hizi, kwa hivyo itakuwa na sifa ya ugeni kuambatana na mpango huu wa uhusiano wa kilugha.

Lugha zilizomo ndani ya aila moja zinakurubiana zaidi kuliko zilizo nje ya aila hiyo. Kwa mfano, Kigikuyu kinahusiana zaidi kimaumbile au kiujenzi na Kiswahili kuliko uhusiano wake na Kimaasaai.

Halikadhalika, Kidholuo nacho kimekurubiana zaidi na Kiacholi kuliko Kigiriama. Hivyo ni kuwa misingi ya lugha zilizohusiana zasemekana zimetokana na ‘kizazi’ kimoja katika asili na usuli. Ndipo kukapatikana mti mnasaba wa uhusiano wa lugha na matawi kadhaa ya kilugha.

Basi iwapo lugha hukabiliwa na vishindo vya mabadiliko katika maisha yake, na iwapo lugha imefungamana na mbinu za kifikira, mawazo na utamaduni wa jamii, basi kukutana kwa lugha mbili, mbali na tija ya kuzuka maneno mapya tu, pia huzuka athari za kifikira, mila, n.k.

Ukweli huo basi, unatutanabahisha kuwa kubadili lugha kwa kuchagua lugha moja, kama Kiingereza, kuwa ndio lugha teule katika kuendesha shughuli za nchi, ni kukaribisha athari nyingine zinazodandia lugha kimawazo na kitamaduni.

Tukumbuke kuwa mabadiliko ni miongoni mwa tarehe ya mwanadamu pamoja na lugha yake, na kuzuilika kwa haya ni muhali katika mjadala huu.

Muhimu ni kuweka mipaka kati ya kutumia lugha kama kifaa, na kuivamia lugha hadi kuipa nafasi ya kuitenga nyingine; na kufafanua baina ya kuifundisha lugha mpya ya kigeni kwa lugha ya kienyeji, na kufunza lugha ya kigeni kwayo.

Mabadiliko

Ni katika ufafanuzi huu tutakapoona sifa tofauti za athari za lugha juu ya jamii zikidhihiri na kubainika zaidi. Ndipo tutakaposisitiza kuwa hali ya kuzorota ya kitamaduni hutokea si kwa kung’ang’ania mila na lugha ya asili, au kupinga kwa kijinga athari mpya za kilugha na nyinginezo ziletwazo na mabadiliko, bali kuzorota huko huletwa na kubadilisha asili kwa mapya yenye athari za kuzorotesha na hata kuathiri maendeleo.

Haikubaliki kuwa kuikuza na kuindeleza lugha ya Kisamburu kwa mfano, au ujuzi na maarifa ya utamaduni huo inamlazimu Msamburu ajifunze Kiingereza pengine mpaka amshinde mwenyeji wa lugha hiyo. Hivyo ni kama kusema kuendeleza ujuzi, maarifa ama fasihi ya Kiingereza, kunamlazimu mtu aende Samburu akajifunze Kisamburu cha kupindukia kwanza ndipo Uingereza wake utimie na kufana.

“Asomaye, asemaye na aandikaye katika lugha yoyote iwayo, uhodari wake katu hauongezi kitu chochote kiwacho katika lugha yoyote nyingine isipokuwa ile ile aliyoitumia”.

Hivyo ni kujibumburusha kuwa wataalamu na waandishi maarufu wa eneo letu la Afrika, Wole Soyinka na Chinua Achebe wakiandika vitabu vyao kwa Kiingereza, basi kubwa walilotimiza ni kuitajirisha na kuikuza lugha hiyo hiyo wala si Kiyomba au Kiigbo.

Wakati ule ule uliotumika kujijenga na lugha isiyokuwa yao, na kupata ‘nishani’ adhimu kwa ladha na uzito wa maandishi yao, nafasi hiyo ingekuwa imetumika bora zaidi lau wangeandika kikwao – ikiwa waliazimia kustawisha na kuendeleza fasihi zao walipoanza uandishi wao.

Kujua na kutumia vilivyo lugha yoyote iwayo, ni mfano wa kufungua mlango wa kuufahamu ulimwengu wa wenye lugha hiyo.

Na zaidi, ni kuendelea pia kuvuta korombojo nyingine zilizotatizana na lugha, kama vile thamani geni, japo hayo yangetendeka bila ya kusudi. Basi kuisoma lugha hadi kumshinda mwenyeji wa lugha wa kawaida, ni njia ya kumiliki (na kumilikiwa na) mawazo, utamaduni na fikira zilizoambatana na lugha hiyo.

Nguvu ya lugha mara nyingi ipo matumizini. Lugha haikutengezwa na wenyewe ili ipambe, ifurahishe au itosheleze thamani za kimila au kitamaduni za wageni wajao kuitafuta lugha yenyewe, bali ni chombo cha kuandalia thamani za kijamii na ni wenzo wa kuendeleza ujuzi si kwa mgeni wa hiyo lugha tu, bali pia mwenye lugha husika.