Wabunge nao wamchoka Spika Wetang’ula, wataka aende
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amejipata mashakani kutoka kwa wabunge wanaokosoa mtindo wa uongozi wake huku baadhi wakitaka ang’olewe mamlakani.
Aidha, wametoa wito kwa muungano wa Kenya Kwanza Alliance, hususan chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Party (UDA) kumtimua Kiongozi wa Wengi Bungeni iwapo Bunge litarejelea hadhi yake.
Wabunge hao wanahoji kuwa matukio yaliyofuatia kura iliyopigwa Jumanne iliyopita kuhusu Kusomwa kwa Pili kwa Mswada wa Fedha, yanaashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya Spika na wabunge, hali inayovurugwa zaidi na mtindo wake wa kuongoza Bunge la Kitaifa.
Mbunge Maalum ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha za Umma (PAC) John Mbadi amemtaja Bw Wetang’ula kama kiini cha matatizo yanayoandama Bunge akimshutumu kwa kuua mjadala na ubaguzi.
“Hatuna tena mjadala bora jinsi ilivyokuwa hata katika enzi za chama kimoja kuanzia 1992. Chini ya Spika Francis Ole Kaparo 1992, 1997 na 2002, wabunge walipata fursa sawa ya kusikika kwenye mjadala Bungeni ikiwemo wanaopinga,” alisimulia mbunge huyo wa zamani, Suba Kusini.
Mbunge wa Kitui Mashinani, David Mwikali, ametoa wito kwa Rais kuwatimua viongozi wa Bunge akianza na Spika na Viongozi wa Wengi.
“Matukio yanayojiri Bungeni yanathibitisha kuwa Wakenya wamepoteza imani na waliowachagua. Kambi ya Walio Wachache ulilemewa na Walio Wengi lakini watu wametuonyesha vinginevyo,” alisema Bw Mboni.
Seneta wa Kaunti ya Nandi, Samson Cherargei, vilevile ameashiria kuwa Spika amefeli Bunge kama mwenyekiti wa Tume ya Huduma ya Bunge (PSC) na ni mwepesi kuwanyamazisha wabunge wanaozua maswali.
Kifungu 106 cha Katiba kuhusu Spika na Manaibu wa Spika Bungeni kinatoa mwongozo kuhusu uchaguzi na utimuaji kuambatana na Kanuni za Bunge la Kitaifa.
“Afisi ya Spika au Naibu Spika itasalia tupu – ikiwa Bunge husika litaafikiana kwa pamoja likiungwa mkono na kura za angalau thuluthi mbili ya wanachama wake,” kinaeleza kijisehemu cha Kifungu 106.
Baadhi ya viongozi hasa katoka Kenya Kwanza waliochelea kutajwa vilevile walielezea kutoridhishwa kwao na matukio ya Jumanne huku wakishutumu viongozi kwa kujipiga kifua na ukaidi.
Kando na Bw Wetang’ula, wanataka Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah na Kiranja wa Wengi Silvanus Osoro watimuliwe.
Ingawa uvamizi wa Bunge na waandamanaji Jumanne dhidi ya Mswada wa Fedha 2024 ulizidisha masaibu ya Bw Wetang’ula, matatizo yake yalianza mwanzoni mwa Bunge la 13 wakati muungano wa Azimio la Umoja ulitofautiana na uamuzi wake uliotangaza Kenya Kwanza kuwa na idadi kubwa ya wabunge.
Wabunge wa Azimio walifululiza nje wakimshutumu Bw Wetang’ula kwa udikteta.