Habari za Kitaifa

Gen Z waadhimisha Siku ya Saba Saba kuwakumbuka waandamanaji mashujaa waliouawa

Na JESSE CHENGE July 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KWA siku muhimu kama hii, Gen Z wanaendelea kukusanyika katika hifadhi ya Uhuru jijini Nairobi kuadhimisha Siku ya Saba Saba, kuwakumbuka mashujaa wenzao walioaga dunia nchini katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024. 

Kwa kutumia mada kama vile #SabaSabaMarchForOurLives inayovuma mitandaoni, inalenga kuwapa heshima waandamanaji shujaa wa zamani na kuhamasisha kwa ajili ya mustakabali bora.

Aidha, tutumie wakati huu kuwaombea na kusaidia familia zilioathiriwa na vifo vya hivi karibuni wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

“Siku ya Saba Saba ni ukumbusho wa nguvu ya wananchi na umuhimu wa kupigania haki zetu. Tunasimama juu ya mabega ya wale waliotutangulia na ni jukumu letu kuendeleza urithi wao,” anasema Amina, mwanaharakati wa Gen Z.

Hapo awali, Saba Saba iliyofanyika tarehe 7 Julai 1990, na ilikuwa na umuhimu katika historia ya Kenya. Wananchi waliandamana kutoka mitaani tofauti kudai mageuzi ya kisiasa na kumaliza utawala wa chama kimoja. Maandamano hayo yalikabiliwa na ukatili kutoka kwa serikali na kusababisha vifo na majeraha kadhaa.

“Leo hii, tunabeba roho ya umoja tunapokusanyika katika hifadhi ya Uhuru kuadhimisha tukio la kihistoria na kuhamasishana kwa masuala yanayotuhusu,” anasema Brian, mwanaharakati mwingine.

Hifadhi ya Uhuru ndipo maandamano ya Saba Saba ya hapo awali yalifanyika ndiposa pana umuhimu maalum kwa Gen Z kukusanyika mle. Linatumika kama ukumbusho wa sadaka zilizofanywa na wale waliojitolea kupigania uhuru wa kisiasa na haki za kidemokrasia.

“Tunataka kuunda nafasi salama kwa ajili ya mazungumzo na ushirikiano. Hili si eneo tu la kimwili, kwani linawakilisha ishara ya matumaini na mabadiliko. Tunataka kuadhimisha urithi huo kwa kusimama pamoja na kudai mistakabali bora,” anasema Grace.

Heshitegi #SabaSabaMarchForOurLives limepata umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, likiongeza ushirikiano na kueneza uelewano kuhusu tukio hili.

Kizazi cha Gen Z kinatumia majukwaa yao ya kidijitali kuhamasisha vijana wenzao na kuhimiza ushirikiano katika maadhimisho haya.

“Kupitia nguvu za mitandao ya kijamii, tunaweza kuongeza sauti zetu na kuvuta tahadhari kwa masuala yanayotuhusu,” anaelezea John, mshawishi wa Gen Z.

“Tuna uwezo wa kuungana na kuhimiza kama babu zetu hapo awali, na siku ya leo ni mfano mzuri wa hilo,” aliongeza.

Wakati kizazi cha Gen Z kinakusanyika katika hifadhi ya Uhuru jijini Nairobi leo, hawatatukuza tu watu shujaa waliojitolea kupigania uhuru unaowanufaisha bali pia wenzao waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.