Habari za Kaunti

Sakaja atenga bajeti kubwa akitarajia pesa kimiujiza


GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja ametia saini Mswada wa Fedha 2024/25 ambao ni wa bajeti ya Sh43.56 bilioni.

Hii ndiyo bajeti kubwa zaidi kuwahi kutengewa shughuli za kaunti tangu mfumo wa ugatuzi ukumbatiwe nchini.

Bajeti hiyo iliwasilishwa kwa Bunge la Kaunti na Waziri wa Fedha Charles Kerich.

Kinaya ni kuwa nusu yake (Sh22.5 bilioni) itategemea wafadhiIi nayo mapato yanayokusanywa na kaunti yanakadiriwa yatafikia Sh20.06 bilioni.

Bajeti hiyo inakuja wakati ambapo maswali yameibuka kuhusu ufisadi ambao umepiga kambi katika Kaunti ya Nairobi.

Gavana Sakaja amekuwa akikashifiwa kutokana na safari zake nyingi za ng’ambo anazodai ni za kimaendeleo ilhali mambo yamesalia yale yale.

Serikali ya Bw Sakaja imetenga Sh838 milioni kujenga na kukarabati masoko, nayo Bunge la Kaunti limetengewa Sh3.56 bilioni kutumika katika wajibu wake wa kufuatilia utendakazi wa gavana.

Aidha, zaidi ya Sh287 milioni zimetengewa ujenzi wa afisi za wadi na kaunti ndogo ili kuleta huduma karibu na wananchi.

Pia, kaunti itatumia Sh120 milioni kujenga vituo vya kuweka vifaa vya kuzimamoto Kangemi, Jamuhuri na Gikomba.