Makala

Mwanafunzi bora wa KCSE Kwale akosa karo ya kusomea Udaktari

Na SIAGO CECE July 19th, 2024 2 min read

WAKATI matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka 2023 yalipotangazwa, Suheil Mumba alijawa na furaha sana.

Alikuwa miongoni mwa wanafunzi bora katika Shule ya Upili ya Kwale huko Matuga, baada ya kupata alama ya A-.

“Nilikuwa na matarajio ya kupata alama ya A, lakini nilipogundua kuwa bado naweza kufanya kozi yangu niliyopenda ya Udaktari na Upasuaji, nilishukuru na kuchukua fursa hiyo,” Suheil alisema.

Alituma ombi lake la kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton na kwa bahati nzuri kupokea barua ya kujiunga na chuo hicho.

Katika barua hiyo, Suheil anatakiwa kuanza masomo yake ya chuo kikuu Agosti 19, 2024, lakini ada ya Sh490,940 kwa mwaka wa kwanza imepunguza furaha ya kijana huyo wa miaka 19 ya kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari.

Haya yanajiri huku kukiwa na mfumo mpya wa kulipa karo ya chuo kikuu nchini ambao umeathiri wanafunzi wengi waliotoka katika familia zisizojiweza.

Suheil Mkalla akiwa nyumbani kwao katika kijiji cha Kombani, Kaunti ya Kwale. Ameomba wahisani kumsaidia kutimiza ndoto yake ya udaktari. Picha| Siago Cece

Suheil anasema amepambana na mawazo ya kujitia kitanzi baada ya kugundua kuwa huenda asiweze kufanikisha fursa pekee ya kutimiza ndoto yake tangu utotoni.

“Nimeomba mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu (HELB), lakini natakiwa kusubiri kwa siku 105 kabla ya kupata majibu. Ninahitajika kujiunga na shule mwezi ujao na nimekosa karo inayohitajika. Nimevunjika moyo na nashindwa kutazama jinsi wazazi wangu wanavyoteseka kwa ajili yangu,” alisema Suheil.

Wazazi wake hufanya kazi ya vibarua katika mtaa wao katika kijiji cha Kombani, Kaunti ya Kwale.

“Wazazi wangu hawawezi kulipa ada na naona hakuna njia nyingine watakayopata pesa. Hawawezi kuchukua mikopo. Sina uhakika kama nitaenda shule. Tunasumbuka hata kupata chakula kwa familia yetu kila siku,” alisema.

Mama yake, Tatu Mohammed alisema kwamba afya yake ya akili na mwili imezorota kutokana na shinikizo la kuhakikisha kwamba mwanawe anajiunga na chuo kikuu.

Suheil sasa anatafuta msaada kutoka kwa wahisani watakaomsaidia kusafiri kwenda Chuo Kikuu cha Egerton Main Campus huko Njoro, na pia kuhudumia mahitaji ya elimu kwa kozi hiyo ya miaka sita.

Baba yake, Rashid Mumba anaweza kupatikana kupitia 0112-982-402.