Habari za Kaunti

Wabunge bado wakabiliwa na wakati mgumu kwa kuunga mkono mswada

Na LUCY MKANYIKA July 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kura ya Mswada wa Fedha uliokuwa na utata, wabunge watatu katika Kaunti ya Taita Taveta wanakabiliwa na mawimbi ya kisiasa kwa kuuunga mkono.

Bw Peter Shake (Mwatate), Bw John Bwire (Taveta), na Bi Lydia Haika (Mwakilishi Mwanamke) waliunga mkono mswada huo wenye utata, uamuzi ambao umewasha moto na kuleta chuki ya kisiasa kwa wapiga kura wao.

Mbali na kutumiwa jumbe za kuwakejeli baada ya namba zao za simu kuwekwa mtandaoni, wanakabiliwa na upinzani haswa kwa wafuasi wao katika kaunti hiyo.

Kwa hofu ya ghadhabu ya umma, wamejiondoa kutoka mitandao ya kijamii na kufutilia mikutano ya hadhara ili kuepuka ghadhabu ya wananchi.

Wabunge hao ambao nyota zao za kisiasa zilikuwa zinang’aa sasa wanahofia mstakabali wao wa kisiasa kutokana na uamuzi wao bungeni.

Hivi majuzi, shule moja huko Mwatate, ililazimika kuhairisha siku ya kutoa tuzo kwa wanafunzi wao bora, ambapo Bw Shake alitarajiwa kuwa mgeni rasmi, kutokana na vitisho vya vijana wenye hasira.

Kwa jitihada za kujikomboa kisiasa, mbunge Shake mnamo Alhamisi alilazimika kufanya mkutano na waendeshaji bodaboda katika Ukumbi wa CDF wa Mwatate, ambapo walimkabili na vilevile kudai Sh2,000 kila mmoja kama posho ya kuhudhuria.

Waendeshaji bodaboda zaidi ya 300 walipewa Sh1,000 kila mmoja baada ya mbunge kusema hicho ndicho kiasi alichokuwa nacho. Polisi walilazimika kupiga doria ili kuzuia fujo.

Aidha, walimtaka mbunge huyo kueleza kilichompelekea kuunga mkono mswada huo wakati wapiga kura wake walikuwa kinyume nao. Pia wanamtaka Bw Shake kufuta kazi maafisa watano kutoka ofisi yake ya ubunge.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Kennedy Domino, waendeshaji bodaboda hawakuficha hisia zao.

“Matakwa haya hayana mjadala tunataka yatekelezwe mara moja. Ako na hadi Agosti 30 kuyashughulikia la sivyo ataoana cha mtema kuni kisiasa,” Mwendeshaji bodaboda Paul Nyambu alisoma matakwa yao kwa mbunge huyo.

“Nataka kuweka wazi kuwa pesa tulizopewa si hongo kwani sisi tulifunga kazi zetu twende kumsikiza. Hatungefanya hivyo bure,” Bw Nyambu aliambia Taifa Leo.

Akijitetea katika kikao hicho, Bw Shake alisema kuwa aliunga mkono mswada huo ili kuleta maendeleo katika eneo hilo, kwani barabara iliyokwama ya Bura-Mghange-Mbale-Mtomwagodi ni miongoni mwa miradi aliyolenga kutekelezwa na serikali.

“Kwa kuwa wananchi hawakuridhishwa na uamuzi wangu naomba radhi kwa hilo,” akasema.

Inaaminika anamezea mate kiti cha ugavana, lakini matukio yanayoendelea yameathiri matumaini yake.

Wakati wa maandamano ya vijana yaliyopita mjini Voi, biashara zake ikiwa ni pamoja na duka la jumla, nyumba yake na mali zingine zilikuwa zimelengwa na hivyo kulazimisha polisi kulinda mali zake ili kuzuia uvamizi.

Wakati huo huo, mwenzake wa Taveta, Bw Bwire, alikumbana na dhoruba kama hiyo kutoka kwa wapiga kura.

Hivi karibuni, alijitokeza tena na kuomba msamaha na sasa anashughulikia kuzindua miradi inayotekelezwa kupitia hazina ya NG-CDF katika eneo bunge lake.

“Nilijifunza kuwa habari mbaya inasambaa haraka kuliko habari njema, makosa yako ni wazi zaidi kuliko matendo yako mazuri, na ulimwengu daima utakukumbusha yale mabaya kuliko mazuri. Ni muhimu kuendelea kuwa na imani, kulinda ushuhuda wako, na kuendelea kutenda mema,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Hata hivyo, baadhi ya vijana wa eneo hilo wamekuwa wakifanya maandamano wakimtaka mbunge huyo kuwajibika na kuweka wazi matumizi ya fedha za NG-CDF.