Wasameheeni mawaziri kwa kuringa- Mwaura
MSEMAJI wa Serikali Isaac Mwaura ameomba Wakenya msamaha, kwa niaba ya serikali kutokana na mienendo ya baadhi ya maafisa wa serikali kuanika utajiri na kuonyesha kiburi hadharani.
Alitoa hakikisho kuwa kitendo kama hicho hakitarudiwa tena chini cha utawala wa Rais William Ruto kwani kinaipa serikali sifa mbaya.
“Kwa niaba ya afisa yeyote wa serikali ambaye ameonekana kujionyesha utajiri wa kupindukia, majigambo na kiburi, ningependa kuwaomba Wakenya msamaha. Aidha, ningependeka kutoa hakikisho kuwa kuanzia sasa maafisa wa serikali, haswa wale wanaoshikilia nyadhifa za juu, watakuwa wanyenyekevu na kuonyesha uwajibikaji kulingana na maagizo yaliyotolewa na Rais,” Bw Mwaura akaeleza jana kwenye kikao na wanahabari katika jumba la KICC, Nairobi.
Aliyekuwa Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen ni mmoja wa mawaziri waliotajwa na vijana, wakati maandamano yao ya kupinga serikali, kama alijigamba hadharani kwa kwa kuvalia mavazi, viatu, mishipi, saa na vitu vingine vya bei ghali kupita kiasi.
Walidai kuwa waziri huyo alikuwa akitumia pesa za umma kujitajirisha huku Wakenya wengi wakiishi kwenye lindi la umasikini kiasi cha kukosa chakula na maji.
Aidha, wakati wa mdahalo kati ya vijana hao katika jukwaa la mtandao wa X, wengi waliwasuta Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha Kuria Kimani kwa kujawa na kiburi wanajibu malalamishi ya wananchi.
“Nimewasikia. Hawa ni wanasiasa vijana ambao nimekuwa nikiwalea ili waweze kuwa viongozi waliokomaa. Nitawashauri kukoma kuwaonyesha wananchi kiburi bali wawe wanyenyekevu kwani ninyi wananchi ndio waajiri wao,” Rais akawajibu vijana hao mnamo Julai 4.
Aidha, Dkt Ruto alitumia jukwaa hilo kuwahakikishia vijana hao wa Gen-Z kwamba serikali itatekeleza mikakati yote aliyotoa ya kupunguza matumizi ya pesa za umma kama vile kupitia safari nyingi katika mataifa ya nje, kuondolewa kwa mgao wa fedha kwa shughuli zisizo za dharura kama vile ukarabati wa Ikulu na Afisi za Naibu Rais na kusikishwa kwa mpango wa ununuzi wa magari mapya.
Wakati huo huo, Bw Mwaura amefichua kuwa msururu wa maandamano ya vijana yaliyoanza Juni 18, 2024 yamechangia hasara ya kima cha Sh6 bilioni kwa wafanyabiashara na taifa kwa ujumla. Hii ni kulingana na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA)
“Tungependa kuwapa pole wafanyabiashara nchini kwa kupata hasara kubwa wakati wa msururu wa maandamano ya vijana kwani kwa ujumla taifa lilipata hasara ya kima cha Sh6 bilioni ndani ya muda huo,” akasema.
Miongozi mwa biashara zilizoporwa na wahuni wakati wa maandamano hayo kote nchini na maduka ya jumla (supermarket), mikahawa, vituo vya kuuza gesi za kupikia, miongoni mwa biashara zingine.
Aidha, mali ya thamani kubwa iliharibiwa waandamanaji walipovamia majengo ya Bunge la Kitaifa na Bunge la Kaunti ya Nairobi yalipovamiwa na waandamanaji mnamo Juni 25, 2024.
Msemaji huyo wa Serikali pia alielezea kusikitishwa kwake na visa ambapo baadhi ya maafisa wa polisi walivamia wanahabari waliokuwa wakipeperusha habari wakati wa maandamano.
Aidha, aliomba msamaha kufuatia kisa cha Jumatano ambapo mwanahabari mkongwe Macharia Gaitho alikamatwa kimakosa na maafisa wa polisi.
“Kwa hivyo, nawaomba enyi wanahabari kusitisha mpango wenu wa kufanya maandamano Jumatano ijayo kulalamikia visa kama hivi. Nawahakikishia kuwa kitendo kama vile kupigwa risasi kwa mwenzenu kule Nakuru na kukamatwa kimakosa kwa Macharia Gaitho havitashuhudiwa tena,” Bw Mwaura akasema.