Ruto aepuka kisiki cha sheria kwa kuagiza mawaziri aliorejesha kazini kupigwa msasa
RAIS William Ruto ameonekana kuruka kisiki cha kisheria kwa kusema kuwa mawaziri aliorudisha kazini lazima watapigwa msasa na bunge la kitaifa kwanza.
Wanasheria walikuwa wamekosoa hatua ya kurejeshwa kazini kwa mawaziri hao wakisema baada ya kufutwa kazi hawafai kushikilia nyadhifa za umma.
Aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya Nelson Havi alisema kuwa kufutwa kazi kwa Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa zamani Justin Muturi, kuliwafanya ‘kutostahili kushikilia wadhifa wowote wa umma milele uwe wa kuteuliwa au kuchaguliwa’.
“Wako katika tapo sawa na magavana walioondolewa mamlakani au majaji wanaopatikana kuwa hawafai kuhudumu. Hiyo ndiyo sheria,” alisema Bw Havi baada ya ilani kuchapishwa katika gazeti la serikali kutangaza kufutwa kazi kwa mawaziri na kuteuliwa.
Katika ilani hiyo, Rais Ruto alimteua Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kaimu waziri katika wizara zote.
Hisia za wataalamu wa sheria ni kuwa mawaziri hao walikuwa wamekosolewa vikali na waandamanaji walioshinikiza kutimuliwa kwao wakidai wanahusika na ufisadi na wanamajitatapo badala ya kufanya kazi.
Mawakili wanasema kuwa kurejesha baadhi ya mawaziri kazini kunafanya uteuzi wao kuwa mpya na wanapaswa kupigwa msasa kana kwamba hawajahi kuteuliwa japo walirudishwa katika wizara walizokuwa wakishikilia kabla ya kufutwa kazi isipokuwa Bi Rebecca Miano aliyeteuliwa Mwanasheria Mkuu.
Kabla ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa, Bi Miano alikuwa waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda.
Wakili Ahmednasir Abdullahi alikubaliana na Havi, akisema kwa kuvunja baraza la mawaziri Rais Ruto alinamaanisha hakuridhika na utendakazi wao.
Alipokuwa akiwatimua mawaziri wake wote na Mwanasheria Mkuu Ruto alisema kwamba alikuwa amefanya ‘tathmini kamili ya utendakazi’ wa baraza lake la mawaziri
Magavana waliotimuliwa, kama Mike Sonko (Nairobi) na Ferdinand Waititu (Kiambu) na majaji, hawawezi kushikilia nyadhifa za umma.