Habari za Kitaifa

Gen Z mnikome-Ruto

Na VITALIS KIMUTAI na CECIL ODONGO July 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto jana aliwaonya vikali Gen Z wanaoandamana nchini kuwa yupo tayari kukabiliano nao, akisema amejaribu kuwa na maelewano kuhusu matakwao yao lakini ni dhahiri nia yao ni kusambaratisha utawala wake.

Kiongozi wa nchi jana alisema hatakubali nchi itekwa na vijana hao na sasa lazima taifa lisonge mbele kutoka kwa utata wa kisiasa ambao umekuwa ukishuhudiwa kwa kipindi cha mwezi moja uliopita.

“Hao waandamanaji walisema niondoe Mswada wa Fedha 2024/25, nikafanya hivyo, kisha wakasema niandae mazungumzo. Walinialika nishiriki kikao nao kwenye mtandao wa X lakini wakatoroka nilipokubali,” akasema Rais Ruto.

“Wanasema wao hawana ukabila, miegemeo ya vyama au sura. Nimempa kila mtu nafasi ya kusema kile alichotaka kusema lakini hatuwezi kuendelea hivi. Lazima tusimame pamoja na kulinda nchi yetu kwa sababu Kenya ni taifa lenye demokrasia,” akaongeza.

Rais alikuwa akihutubia wananchi katika Shule ya Msingi ya Kipsonoi baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapoli kwenye Kanisa la AGC Chebango, Kaunti ya Bomet.

Usemi wake mkali unakuja wakati ambapo Gen Z wametangaza kuwa wataandaa maandamano wanayodai yatakuwa  makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini hapo kesho.

Gen Z  wanadai Rais anawachezea shere baada ya kutangaza nusu ya baraza lake la mawaziri. Mnamo Ijumaa iliyopita, Rais Ruto aliwarejesha mawaziri sita waliokuwa wametimuliwa hapo awali kutokana na maandamano na shinikizo za vijana hao

Akionekana kuwa tayari kuwakabili waandamanaji, Rais alisema hatavumilia maandamano zaidi akidai kuwa yanafadhaliwa dhidi ya utawala wake.

“Nataka kuwaahidi kuwa maandamano hayo lazima yakome. Yametosha. Wale ambao wanaendelea kuvumisha maandamano haya wajitokeze na watuambie wanalenga kutimiza nini na wafadhili wao watafanya nini baada ya ghasia hizi,” akasema Rais Ruto.

Tangu maandamano hayo yaanze mwezi moja uliopita, zaidi ya watu 50 wamefariki, uharibifu wa mali umetokea huku majengo ya bunge nayo pia yakivamiwa.

“Tutapambana na wale ambao wanazua ghasia, kuharibu mali ya watu na kusababisha vifo vya Wakenya huku pia wakipora mali. Tuna serikali ambayo ina wajibu wa kuwalinda raia na mali na tutafanya hivyo,” akasema.

Mitandaoni vijana na wanasiasa walimkabili Rais, wakisema kuwa hawaogopi kupigania haki yao hata itawapo mauti yatatokea.  Kinara wa Narc Kenya Martha Karua alimkemea Rais akisema ‘anafikiria nchi ni mali yake’ na enzi za uongozi wa kidikteta zilipitwa na wakati.

Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Martin Andati, kauli ya Rais Ruto na sasa amezua ghadhabu na kuwapa mori zaidi za vijana kupigania mageuzi.

“Raila amemruka Ruto na hivyo vitisho vya Rais sasa vimefanya mambo yamekuwa magumu. Hata kama ni kuwaua, huwezi kuwamaliza wote ila tu pengine unataka Kenya ishuhudie mauaji ya halaiki,” akasema Bw Andati

Hotuba ya jana ilikuwa mara ya kwanza kwa rais baada ya kuteua baraza lake la mawaziri ambalo limezua ghadhabu sana miongoni mwa Gen Z.

Juhudi za Rais za kuunda serikali ya muungano ambayo ingeshirikisha wandani wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga nazo zimegonga mwamba baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kujiondoa kwenye mazungumzo na mipango hiyo.

Jana, Rais alionekana kumakinikia pia maadai kuwa maandamano hayo yanafadhiliwa siku chache tu baada ya kudai kuwa Wakfu wa Ford umekuwa ukiyafadhili.

Shirika hilo nalo limekanusha hilo na kutoa orodha ya miradi ambayo inafadhili nchini ikiwemo ile ambayo imekuwa ikisimamiwa na afisi ya Rachel Ruto, mkewe Rais.

Aidha Waziri Mteule wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki aliwahi kunukuliwa kabla ya kutimuliwa afisini kuwa kulikuwa na uchunguzi ambao ulikuwa ukiendelea dhidi ya baadhi ya wanasiasa kwa kufadhili ghasia na maandamano nchini.