Habari za Kaunti

Wakulima wa miwa wataka AFA ilainishe mpango wa malipo kwa wakulima


WAKULIMA wa miwa wameitaka Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) kuandaa mpango bora wa utoaji malipo kwa wakulima, la sivyo hawatawasilisha miwa yao kwa kampuni za sukari.

Haya yanajiri wakati ambapo wakulima wanalalamikia kupata hasara kubwa wakati wa kuvuna na kusafirisha miwa hadi viwandani.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Miwa Nchini (KSGA), Richard Ogendo alisema kuwa kwa jumla wakulima wa miwa nchini hutozwa ada haramu ya Sh3 milioni kila mwaka kusafirisha miwa yao kutoka shambani hadi viwandani.

“Ningetaka kuwajulisha kwamba wakulima wanabebeshwa mzigo wa ada haramu ya wakati wa kuvuna na kusafirisha miwa hadi mashambani. Hatutavumilia ada kama hii,” akasema Bw Ogendo.

Katika barua ya KSGA kwa AFA, wakulima wanapendekeza kuwa mamlaka hiyo ibuni mikakati itakayosaidia viwanda vya miwa vinavyomilikiwa na serikali kununua angalau trekta 40 za kusafirisha miwa na viajiri wavunaji na wapakiaji zao hilo.

“Aidha, tunaitaka serikali kuanzisha vituo vya kupima uzani wa miwa katika maeneo yote kunakokuzwa zao hilo nchini Kenya. Hii itawaondolea wakulima usumbufu mwingi wanaoupitia haswa katika eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu,” Bw Ogendo akaongeza.

Katibu huyo mkuu vilevile aliitaka serikali kuhakikisha kuwa kampuni zake za sukari hazicheleweshi malipo ya wakulima.

“Wakulima walipwe kila wiki kulingana na kanuni inayosimamia kilimo cha miwa nchini,” Bw Ogendo akaeleza.

Katika kaunti ya Migori wakulima wa miwa wametisha kutowasilisha miwa yao viwandani ikiwa hawatalipwa kwa wakati unaofaa.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kitaifa la Wakulima wa Miwa Argweng Adongo alisema kuwa wakulima wanapaswa kulipwa wiki moja na mbili baada ya wao kuwasilisha mazao viwandani.

“Hatutaruhusu kampuni za miwa kuchelewesha malipo ya wakulima kwa muda mrefu zaidi,” akasema Bw Adongo.