Habari za Kitaifa

Usajili upya wa vitambulisho ni kawaida katika nchi kama Uganda – Serikali

Na LABAAN SHABAAN July 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imepuuza malalamishi ya mashirika ya umma kuhusiana na vitambulisho vipya vinavyoendelea kutolewa: ambavyo vitakuwa vikisajiliwa upya kila baada ya miaka 10.

Kadi hizo kwa jina Maisha Namba zilianza kutolewa mwisho wa 2023 zikilenga kufutilia mbali kadi zinazotumiwa sasa.

Watakaosajiliwa watakuwa na namba dijitali ya kipekee ya utambulisho (UPI).

UPI itatolewa wakati wa kuzaliwa, huku Maisha Namba ikitolewa raia anapotimu umri wa miaka 18.

Idara ya uhamiaji ilitoa taarifa siku moja baada ya mashirika ya umma kulalama kwa nini namba hii itasajiliwa kila baada ya miaka kumi.

Hofu ya mashirika haya ni kuwa yamkini kadi hizi zitatumiwa kutimiza njama ya udanganyifu katika uchaguzi.

“Kadi hii ina sehemu ambayo inasomeka kwa mitambo na usajili upya hauendi sambamba na msimu wa uchaguzi mkuu,” ilisema taarifa iliyotiwa sahihi na Katibu wa Idara ya Uhamiaji Julius Bitok mnamo Jumatatu, Julai 22, 2024.

“Kama stakabadhi nyingine kama vile kadi za benki (ATM), Maisha Namba ina kijipande cha kielektroniki (microchip) ambacho huisha baada ya hadi miaka 10,” aliongeza.

Akitetea uhalali na umuhimu wa kadi hii, Bw Bitok alieleza kuwa usajili upya wa vitambulisho ni desturi katika mataifa kama Uganda, Tanzania, Nigeria na Ufaransa.

Kulingana na serikali, watakaosajiliwa upya watapigwa picha ya pasipoti pekee bila kuchukuliwa alama za vidole.

Bw Bitok alisema serikali imenunua mtambo wa kisasa ambao una uwezo wa kuchapisha kadi 30,000 kila siku dhidi ya maombi 10,000 kwa siku.

Mwaka jana, 2023, serikali ilitangaza kuwa shughuli hii itagharimu mlipa ushuru kima cha Sh1 bilioni.

Kulingana na Bw Bitok, kufikia sasa, Wakenya 927,630 wamepokea Maisha Namba.

Shughuli ya usajili inaendelea tangu Februari 2024 baada ya mahakama kuondoa amri iliyosimamisha usajili Desemba 2023.

Shirika la Katiba Institute lilikuwa limewasilisha kesi kortini kuzuia mchakato huu ambao unaendeshwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.