Habari za Kitaifa

Jamii ya Maa yamtetea Soipan dhidi ya dhuluma mtandaoni

Na FRIDAH OKACHI July 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MUUNGANO wa wanawake kutoka jamii ya Masai (Maa Women’s Network) umekemea lugha mbovu inayotumiwa kwa Waziri Mteule wa Ulinzi Soipan Tuya kwenye mitandao ya kijamii baada ya Rais William Ruto kubadilisha jina lake kutoka Waziri wa Mazingira hadi Waziri wa Ulinzi.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Kiongozi wa Muungano wa Wanawake Bi Angeline Yiamiton Siparo alisema wanawake wa jamii hiyo wamekosewa heshima kutokana na lugha, picha na video ambazo zinasambazwa mitandaoni zikielekezwa kwa Bi Soipan.

“Tunakemea matusi ya aina yoyote ambayo yanaelekezwa kwa mama wa jamii yetu. Hii kunionyesha dharau na kutomheshimu Bi Soipan,” alisema Bi Siparo.

Hata hivyo, kundi hilo lilimpongeza Rais William Ruto kwa uteuzi huo, wakitaja binti huyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo.

“Bi Tuya ni kiongozi ambaye alichanguliwa kuwa mwakilishi wa kike katika Kaunti ya Narok kwa kipindi cha miaka 10. Tuna imani ana uwezo wa kutekeleza jukumu alilopewa na Rais wa Jamhuri ya Kenya,” aliongeza Bi Siparo.

Kundi hilo liliomba mashirika mengine yanayopigania haki za wanawake kujiunga nao na kupinga dhuluma ya mitandao ya kijamii inayoelekezwa kwa Bi Tuya ambaye ni kiongozi wa Taifa na sio wa jamii ya Maa pekee.

“Maisha yake au mahusiano ni mambo ya kibinafsi. Taarifa zinazosambazwa mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii ni madai ya uongo na kumharibia sifa binti wetu,” alisisitiza Bi Siparo.

Bi Soipan Tuya ni miongoni mwa wanawake wanne walioteuliwa katika awamu ya kwanza baada ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa Julai 11, 2024 kutokana na shinikizo la vijana almaarufu Gen Z waliotoa pendekezo hilo. Gen Z walidai kuwa baraza hilo lina mawaziri wafisadi na wazembe wa kutekeleza kazi yao.

Siku za hivi karibuni, Bi Tuya amekashifiwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya utezi wake kubadilishwa kutoka Waziri wa Mazingira na kuwa Waziri wa Ulinzi.