25/06/2019

Man United yasema kamwe haiwezi kutishwa na Arsenal FA

NA CECIL ODONGO

MENEJA wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema kwamba kutanishwa kwa timu hiyo na mabaingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Arsenal ni mtihani mkubwa kwake japo ana imani watapata ushindi katika mechi hiyo ya Shirikisho la Soka nchini Uingereza(FA).

Kabiliano hilo litakutanisha timu hizo mbili ambazo zina ufanishi wa kupigiwa mfano kwenye kombe hilo, Arsenal wakiwa wameubeba ubingwa huo mara 13 nao Manchester United mara 12.

Arsenal maarufu kama ‘The Gunners’ walifuzu raundi ya tatu ya FA kwa kuwabamiza Black Pool inayoshiriki  Ligi ya Daraja la Pili 3-0 huku United wakiwachabanga Reading 2-0.

Solskjaer ambaye yupo kwenye kambi ya mazoezi ya majira ya joto  na timu ya Manchester United jijini Dubai hata hivyo ameeleza kufurahishwa kwake na droo hiyo.

“Ni droo nzuri kwasababu wachezaji wangu wanahitaji mechi ngumu kama hizi ili kustahimili upinzani. Japo kila  mtu anasema tumekuwa tukishinda, hatujapatana na timu zinazotajwa kuwa ngumu,” akasema Mkufunzi huyo.

Manchester United itakabiliana na Arsenal Jumamosi Januari 26 ugani Emirates ili kubaini timu itakayofuzu kwa raundi inayofuata.