Habari

Mahakama ya Rufaa yasitisha mazishi ya ajuza, 102


MAHAKAMA ya rufaa imesitisha kwa siku 30 mazishi ya mzee wa miaka 102 anayeng’ang’aniwa na wake zake wawili Sarah Kathambi na Grace Rigiri Silas.

Majaji Gatembu Kairu, Lydia Achode na Ngenye Macharia waliamuru maiti ya Mzee Silas Kamuta Igweta isalie katika mochari jijini Nairobi hadi kesi iliyowasilishwa na wake zake wawili isikizwe na kuamuliwa.

Kesi hiyo imekuwa mahakamani kwa muda wa miezi mitano sasa.

Wakisitisha mazishi ya Kamuta, majaji Gatembu, Achode na Ngenye walisema, “Rufaa aliyowasilisha Sarah na bintize Purity Kinya na Miriam Makena ina mashiko kisheria.”

Sarah amepinga Rigiri akimzika mume wao akidai walitengana miaka 40 iliyopita na hawana uhusiano wowote.

Kupitia wakili Danstan Omari, Sarah, Kinya na Makena wameeleza mahakama ya rufaa kwamba wamekuwa wakiishi na marehemu na ndio wanastahili kumzika.

Majaji hao wamesema kwamba ikiwa wataruhusu Kamuta azikwe basi itakuwa fedheha kwa familia huku mahakama ikiamuru maiti ifukuliwe kuzikwa tena.

Mahakama Kuu Mei 21 2024, iliwaamuru Sarah na Rigiri wakubaliane atakakozikwa marehemu. Lakini Sarah na dada zake walipinga wakisema kuwa wao ndio wako na idhini ya kumzika Kamuta.

Katika uamuzi wa kihistoria uliotolewa kuhusu kesi hiyo mnamo Februari na mahakama kuu, Sarah aliruhusiwa kumzika marehemu lakini Grace akawasilisha rufaa.

“Mtu akifa yuko na haki ya kuzikwa na mke waliyekuwa wakiishi naye kabla ya kuaga,” hakimu mwandamizi Bw Gerald Gitonga alisema huku akimruhusu Sarah Kathambi, 78, kumzika Silas Kamuta Igweta, 102.

Mwili wa Kamuta uliokuwa umehifadhiwa katika Mochari ya Ummash ulihamishwa na kupelekwa mahala ambapo gharama sikubwa.

Majaji Gatembu, Achode na Ngenye walielezwa kwamba familia ya Sarah imepata gharama ya zaidi ya Sh6.5 milioni.

Kabla ya kuaga alikuwa akiishi na Sarah katika makazi yao ya kifahari Westlands.

Baada ya kuaga mkewe wa kwanza Grace Rigiri waliyekuwa wamefunga ndoa kanisani aliwasilisha kesi akipinga Sarah kumzika Kamuta.

Grace alisema yeye ndiye alikuwa na haki ya kumzika mumewe kama mke wa kwanza katika shamba lake Embu.

Lakini Sarah kupitia mawakili Nelson Kinyanjui, Omari na Shadrack Wambui alipinga Grace kumzika mzee huyo kwani alikuwa amemweleza akiaga amzike yeye (sarah) na watoto wake.

Bw Omari alieleza mahakama kwamba sheria za Kenya hazijafafanua pale mtu aliye na mke zaidi ya mmoja atakapozikwa.

Mawakili hao waliomba mahakama imruhusu Sarah amzike mumewe waliyeishi pamoja kwa zaidi ya miaka 40.

“Kwa miaka zaidi ya 40, Kamuta hakuishi na Grace. Ukweli ni kwamba Grace hamfahamu mumewe waliyefunga ndoa kanisani na walipopeana talaka, Sarah akaolewa kwa mujibu wa sheria za Utamaduni wa Ameru,” Bw Omari alisema huku akimsihi hakimu abadilishe mkondo wa sheria za mazishi.

Bw Omari alisema maiti iko na haki ya kuzikwa pale mfu alichagua akiwa bado hai.