Michezo

Ni kufa-kupona Gathimba akivizia medali Paris 2024

Na GEOFFREY ANENE July 31st, 2024 1 min read

BINGWA mara tatu wa kutembea kwa haraka kilomita 20 barani Afrika, Samuel Gathimba Alhamisi, Agosti 1, 2024 hana fursa ya kuteleza atakapokuwa mawindoni kutafuta medali ya fani hiyo katika Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.

Gathimba, 36, ni mwanariadha wa kwanza kutoka Kenya kujitosa ulingoni kwenye makala hayo ya 33. Alishiriki 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil, akishirikiana na Simon Wachira, lakini wote hawakumaliza.

Mbali na Gathimba na Wachira, Wakenya wengine wanaume wameshiriki fani hiyo ya kutembea kwa haraka katika Olimpiki ni Pius Munyasia mjini Los Angeles nchini Amerika mwaka 1984, na David Kimutai, Justus Kavulanya na Julius Sawe mjini Atlanta nchini Amerika mwaka 1996.

Gathimba akishinda mchujo wa kitaifa uwanjani Nyayo, Nairobi, mnamo Januari 27, 2024. PICHA|MAKTABA

Kimutai na Sawe pia walishiriki makala ya Sydney nchini Australia mwaka 2000. Isitoshe, Kimutai alishiriki makala ya 2008 mjini Beijing, Uchina.

“Nimepata ujuzi mwingi kutoka kwa Olimpiki 2016 na pia mashindano ya Afrika na ninahisi kuwa natosha sasa kupata medali katika mashindano makubwa kama Olimpiki,” akasema afisa wa magereza Gathimba katika mahojiano.

Muda bora wa Gathimba mwaka huu katika kutembea kilomita 20 ni saa moja, dakika 28 na sekunde sita aliandikisha akizoa medali ya fedha kwenye Michezo ya Afrika mjini Accra, Ghana mwezi Machi.

Gathimba anashikilia rekodi ya Afrika ya 1:18:23 aliyoweka Juni 18 mwaka 2021. Alijikatia tiketi yake ya Olimpiki akimaliza Riadha za Dunia mwaka 2023 katika nafasi ya tisa alipotembea 20km kwa saa 1:18:23 mjini Budapest, Hungary.

Ana kibarua kigumu mjini Paris ambapo huenda atakuwa akishiriki Olimpiki yake ya mwisho.

Wanaopigiwa upatu kuwania taji ni pamoja na Mwitaliano Massimo Stano anayetetea taji, bingwa wa dunia Alvaro Martin kutoka Uhispania na Mjapani Koki Ikeda ambaye ana muda bora duniani mwaka huu.