Maafisa watumwa Taita Taveta kutafuta waliotangamana na dereva anayeugua Mpox
SERIKALI imechukua tahadhari zaidi baada ya ugonjwa wa homa ya tumbiri kugunduliwa nchini.
Katibu wa Wizara ya Afya na viwango vya utaalamu, Mary Muthoni, alisema Alhamisi kuwa, mtu mmoja alipatikana na virusi hivyo kwenye mpaka wa Taita Taveta na kutengwa ili atibiwe.
Alisema haya katika Bekam Hotel, Kaunti ya Kirinyaga wakati wa ziara ya kuangazia maendeleo na mafunzo ya Wahudmu wa Afya Mashinani (CHPs) akieleza kuwa wanafuatilia waliotangamana na mgonjwa huyo ili kuhakikisha hautasambazwa nchini.
“Dereva wa trela mpakani aliyepatikana anaugua Mpox amezuiliwa na safari yake kukatizwa, tunajaribu kubaini ni watu wangapi aliotangamana nao,” alisema.
Alifichua kuwa kundi la maafisa wa afya ya umma limetumwa Taita Taveta kusaka waliotangamana na mwathiriwa na kuimarisha uangalizi.
Uangalizi umeimarishwa vilevile katika vituo vyote 32 vya kuingilia mpakani kote nchini, alisema.