Habari za Kitaifa

Mutahi amwaga mtama kuhusu kutoweka kwa Riggy G

Na MWANGI MUIRURI August 2nd, 2024 2 min read

GAVANA wa Nyeri Mutahi Kahiga amedai kwamba kujificha kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Mathira mnamo Mei kulichangiwa na ‘mateso ya kisiasa’ kutoka kwa mrengo wa Rais.

Bw Kahiga amefichua kwamba Bw Gachagua alikuwa akiandamwa na masaibu sawa na yaliyompata Rais William Ruto alivyonyanyaswa na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa Naibu Rais.

Asema ahadi ya Rais ya kumlinda naibu wake dhidi ya kile alichokiita ‘mateso ya kisiasa’  haijatimia na akaongeza kuwa hali hii “inatufanya tushangae ni nini kimemwingia Rais ambaye tulimpigia kura 2022.”

Gavana Kahiga asema Mlima Kenya kwa sasa unajifunza mengi kwa hatua ya  kumwamini Dkt Ruto bila makubaliano ya kimaandishi kabla ya uchaguzi na kuundwa kwa serikali ya Kenya Kwanza.

“Hatukumwendea Ruto kama timu, viongozi wetu wote wakuu katika serikali yake walimwendea kibinafsi. Hatujawahi kuwa na mshikamano katika serikali hii kama Mlima Kenya,” akasema.

“Nilikuwa nimempendekezea Bw Gachagua tushinikize makubaliano ya maandishi na rais au hata tukatize ndoa yetu. Hata hivyo, alipuuzilia mbali pendekezo hilo akisema kwamba aliamini kuwa mambo yangetengenea. Alishikilia kwamba tutasalia katika chama cha Rais cha UDA,” Bw Kahiga aongeza.

Hata hivyo, gavana huyo ameonya kuwa Mlima Kenya una chaguo mbadala akisema “tuna vyama vingi vya kisiasa vya eneo la Mlima Kenya.”

“Rais anajua jinsi alivyoondoka Jubilee mbambo yalipokuwa magumu,” Bw Kahiga amekariri, akirejelea jinsi Dkt Ruto  alivyounda chama cha UDA alipokuwa akijiandaa kuondoka katika chama tawala cha Jubilee kabla ya uchaguzi wa 2022.

Uungwaji mkubwa wa Gachagua Mlimani

Amedai kuwa Gachagua anaungwa mkono na magavana wote wa Mlima Kenya “na ninazungumza kama mwenyekiti wao katika kaunti zote 10.”

Gavana huyo alisema dhuluma za kisiasa  kutoka kwa washirika wa Rais  zilimwathiri Gachagua hadi akalazimika kujificha  ili apate muda wa kutafakari.

“Naibu Rais alitoweka ghafla na hakuna aliyejua alikokuwa. Ilikuwa hali ya kutisha kwani hata hakupokea simu. Binafsi niliongoza juhudi za kumtafuta kwani mambo yaliyokuwa yakimwandama yalikuwa hatari. Baadhi ya viongozi wetu wa serikali walikuwa wameanza kumdharau. Alikuwa akinyimwa usafiri wa ndege za kijeshi, kulikuwa na njama zilizomzunguka na kutoweka kwake kusingechukuliwa kwa urahisi,” alisema.

Mnamo Mei 21 Gachagua alijitokeza baada ya wiki moja ya kutoonekana hadharani na kutangaza kwamba alikuwa ameingia katika msitu wa Mlima Kenya kufunga na kusali.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga akihutubu mwezi uliopita katika hafya iliyowaleta pamoja wafanyakazi wa kaunti hiyo. Mutahi ni mwendani mkuu wa Naibu Rais. Picha|Joseph Kanyi

Jana, Bw Kahiga alisema alipompata nyumbani kwake Mathira, Naibu Rais alikuwa “katika hali ya kutafakari”.

Alidai kuwa kumpata Bw Gachagua hakukuwa rahisi “kwani ilinilazimu kupitia mtandao wa wasaidizi wake ambao ni pamoja na maafisa wa usalama na familia.”

Alipofika nyumbani kwa Gachagua, gavana asema, alipata “mtu aliyefadhaika, akiwa peke yake nyumbani na katika mazungumzo yetu yaliyofuata, nilitambua uzito wa hali aliyopitia.”

Bw Kahiga asema alizungumza na Rais kibinafsi kuhusu masuala hayo.

Alidai mateso hayo yameongezeka hadi kufikia hatua kwamba “Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) inaonekana wazi kuendeleza kisasi dhidi ya Naibu Rais.”

Alikiri kwamba kuna njama ya kumuondoa Gachagua mamlakani

Bw Kahiga alidai njama hizo zinasukwa kwa kisingizio kwamba alihusika na ghasia ambazo zimekumba mji wa Karatina kwa muda wa mwezi mmoja uliopita.

Bw Kahiga amemkosoa mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri kuhusu matamshi yake kuhusu wanasiasa wanaofadhili waandamanaji.

“Ninataka Kiunjuri aeleze vifaa halisi vilivyosafirisha wahuni 25,000 hadi Nairobi kutoka Mlima Kenya na pia ataje jinsi idadi hiyo inaweza kusafirishwa na kwa malori mangapi,” alisema.