Mwanamume ajiua katika seli ya polisi huku mamake akiwa rumande
KATIKA hali ya kusikitisha, mshukiwa alipatikana amekufa ndani ya seli ya polisi katika kituo cha Polisi cha Ramula, kaunti ndogo ya Gem, mnamo Alhamisi.
Marehemu ambaye ametambuliwa kama Fredrick Odhiambo Ochieng’, alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa katika seli za kituo cha polisi cha Ramula.
Alikuwa ameshindwa kuheshimu wito wa mahakama na kusababisha Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Siaya kutoa kibali akamatwe.
Kulingana na ripoti ya polisi ambayo Taifa Leo iliona, marehemu anaripotiwa kujitoa uhai akiwa katika seli za polisi kwa kutumia shati lake.
“Saa 16:30, mahabusu Frederick Odhiambo Ochieng, 40, alijitoa uhai katika seli ya polisi kwa kutumia shati lake. Mwili wa Fredrick Odhiambo Ochieng ulipatikana ukining’inia kwenye dirisha la seli ya kituo cha polisi,” ilisema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo iliendelea kusema: “Alikuwa ametoroka mahakamani mara kadhaa na kibali cha kumkamata kilitolewa dhidi yake. Maafisa kutoka kituo cha polisi cha Ramula walimkamata ili kufikishwa mahakamani kesho. Aliwekwa katika seli kwa muda akisubiri kupelekwa kituo cha polisi cha Yala ambako alijiua kwa kutumia shati lake lililofungwa kwenye vyuma vya dirisha.”
Bw Shadrack Ochieng, nduguye marehemu, alisema familia ilishtuka baada ya kufahamu kisa hicho cha kusikitisha.
Marehemu, ambaye alikuwa mtoro baada ya kushindwa kuheshimu masharti ya mahakama kuhusu kesi ya kushambulia jirani yake, alikuwa nje kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa kiasi sawa.
“Mama yangu alikuwa mdhamini mahakamani, kwa hiyo, baada ya kushindwa kufika mahakamani mara kadhaa, mahakama ilitoa kibali akamatwe. Tunapozungumza, mama yangu yuko rumande kwa sababu ndiye alikuwa mdhamini,” akasema Bw Ochieng.
Aliendelea: “Marehemu ndugu yangu marehemu alikuwa amemshambulia jirani na kumsababishia majeraha makubwa.”
Inasemekana alitoweka kwa wiki kadhaa akaenda na mke wake wa pili Nairobi na baada ya muda, walitofautiana na kuachana.
Baada ya mahakama kutoa kibali na mama yake kukamatwa, ndugu za marehemu walichukua jukumu kubwa la kumtafuta na hatimaye walipompata, kwa msaada wa polisi, akakamatwa.
“Familia ilitaka tu mama yangu mzee ambaye ni mgonjwa atoke nje ya rumande ya polisi, hakufanya uhalifu wowote,” akasema Bw Ochieng.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya kaunti ndogo ya Yala ukisubiri uchunguzi wa maiti.