Omanyala aona vimulimuli katika vita vya kufuzu fainali za 100m Olimpiki
BINGWA wa Afrika na Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022, Ferdinand Omanyala amebanduliwa kwenye vita vya kuwania medali katika Michezo ya Olimpiki baada ya kukamata nafasi ya nane kati ya tisa kwa sekunde 10.08 katika nusu-fainali ya tatu mjini Paris nchini Ufaransa mnamo Jumapili, Agosti 4, 2024.
Ni mara ya pili mfululizo Omanyala amekosa kupita nusu-fainali kwenye Olimpiki baada ya kupigwa breki katika makala ya 32 mjini Tokyo nchini Japan mwaka 2021.
Katika makala haya ya 33, Inspekta wa Polisi, Omanyala, alitinga nusu-fainali kwa kushinda mchujo wa kundi lake katika raundi ya kwanza kwa sekunde 10.08 mnamo Jumamosi, Agosti 3.
Wapinzani wa Omanyala katika nusu-fainali Fred Kerley (Amerika), Kishane Thompson (Jamaica), Andre De Grasse (Canada), Abdul Hakim Sani Brown (Japan), Zharnel Hughes (Uingereza), Abdul-Rasheed Saminu (Ghana) na Benjamin Richardson (Afrika Kusini) walikuwa na muda bora katika raundi ya kwanza kumliko.
Omanyala anayeshikilia rekodi ya Afrika sekunde 9.77 kutoka mwaka 2021 na alikuwa na muda wa pili bora mwaka huu (9.79) nyuma ya Thompson (9.77), alishinda Puripol Boonson kutoka Thailand pekee (10.14).
Thompson na Kerley walijikatia tiketi kushiriki fainali baada ya kukamilisha katika nafasi mbili za kwanza kwa sekunde 9.80 na 9.84, mtawalia.
Oblique Seville kutoka Jamaica (9.81) na bingwa wa dunia Noah Lyles kutoka Amerika (9.83) walinyakua tiketi za fainali moja kwa moja kutoka nusu-fainali ya kwanza.
Nusu-fainali ya pili ilishuhudia Akani Simbine kutoka Afrika Kusini (9.87) na Letsile Tebogo kutoka Botswana (9.91) wakishinda tiketi za moja kwa moja kutoka nusu-fainali ya pili. Bingwa wa Olimpiki 2020 Marcell Jacobs kutoka Italia aliridhika na nafasi ya tatu kwa 9.92.
Fainali pia ni leo usiku (10.50pm).
Nusu saa kabla ya Omanyala kushiriki fainali, Mkenya Zablon Ekwam alishuhudia ndoto yake ya kuwania nishani ya 400m ikiyeyuka baada ya kuhisi usumbufu katika mguu wake wa kulia wakielekea kupiga kona ya mwisho na kusalimu amri. Alikuwa mwakilishi wa pekee wa Kenya katika 400m.