Amerika yaonya Kenya dhidi ya ukatili wa polisi na ukiukaji wa haki za binadamu inapokabili waandamanaji
AMERIKA imeonya serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi kukabili waandamanaji na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Waziri msaidizi wa Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Kibinadamu wa Amerika aliyezuru nchini Uzra Zeya ameelezea wasiwasi mkubwa wa nchi yake kuhusu ukatili wa polisi wa Kenya, akisema ni ukiukaji wa Katiba ya Kenya ya 2010.
Mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili nchini Kenya, Bi Zeya ameitaka Kenya ijitolee kuzingatia sheria na kuheshimu haki za binadamu, kuchunguza visa vya kutoweka, utekaji nyara na kukamatwa kiholela kwa waandamanaji.
Akiwahutubia wanahabari katika Ubalozi wa Amerika kabla ya kuondoka nchini, Bi Zeya alifichua kwamba alisisitiza umuhimu wa uhuru wa kujieleza, kukusanyika na uhuru wa vyombo vya habari ili demokrasia iweze kustawi. Bi Zeya aliyasisitiza haya alipokutana na Rais William Ruto, mashirika ya serikali na maafisa wakuu serikalini.
Shutuma dhidi ya makosa ya serikali kwa raia
“Katika mazungumzo yangu na Rais Ruto na maafisa wakuu wa Kenya, nilishutumu ghasia zilizofanywa dhidi ya waandamanaji waliodumisha amani, watetezi wa haki za binadamu na wanahabari na nikahimiza kulindwa kwa uhuru wa kimsingi wa kukusanyika kwa amani na kujieleza, kama ilivyo katika Katiba ya Kenya,” alisema.
“Pia nilisisitiza umuhimu mkubwa wa vikosi vya usalama kujizuia, kujiepusha na ghasia za aina zote, na uchunguzi wa haraka na uwajibikaji kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu uliotekelezwa na polisi.”
Alisema kuwa ziara yake nchini Kenya ilijiri wakati nchi inakabiliwa na wakati mgumu kwa demokrasia hasa katika kukabiliana na maandamano yanayoongozwa na vijana wakitaka utawala bora na kulalamikia ufisadi.
“Nilimhimiza Rais Ruto kuchukua hatua madhubuti kuhusu ahadi zake za hivi majuzi kwa umma za kuimarisha utawala wa sheria, mipango ya kupambana na ufisadi na kuendeleza uwajibikaji katika serikali yake,” alisema Bi Zeya, saa chache kabla ya maandamano ya ‘Nane Nane’.
“Nadhani suali la msingi ni utekelezaji wa ahadi hizi kwa vitendo. Eneo moja mahususi ni umuhimu wa kuchunguza ripoti za ukatili unaotekelezwa na vikosi vya usalama, kuwashtaki wale wanaopatikana na hatia.”
Mbali na Rais, alikutana na Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Monica Juma, Jaji Mkuu Martha Koome na maafisa wakuu kutoka Wizara ya Usalama wa Ndani na vilevile wakuu wa mashirika na idara za kukabili ufisadi.