Habari za Kitaifa

Polisi watumia kila mbinu kuzima maandamano; wapekua magari, wapita njia wakiwalima marungu

Na WAANDISHI WETU August 9th, 2024 2 min read

SHUGHULI zote zilisimama Nairobi jana baada ya polisi kuamrisha wafanyabiashara kufunga maduka na kuwafukuza watu na magari kutoka katikati mwa jiji katika juhudi za kuzuia maandamano ya kupinga serikali.

Taharuki ilitanda jijini polisi wakiwakabili waandamanaji kwa kuwafyatulia vitoa machozi wasikusanyike walivyopanga na kukita kambi jijini kushinikiza mabadiliko serikalini.

Kuanzia asubuhi hadi jioni, polisi waliwazuia watu kuendesha shughuli zozote huku wakiwatimua wachuuzi na wanabodaboda kwa mijeledi.

Walizunguka katika barabara za jiji wakiwataka watu kufunga biashara zao na kuzuia magari ya uchukuzi kuingia jijini kwa kuweka vizuizi katika maeneo ya kimkakati.

Vizuizi viliwekwa katika mzunguko wa Bunyal, karibu na uwanja wa michezo wa Nyayo ambapo polisi walizuia magari kuendelea na safari hadi kati kati mwa jiji.

Katika barabara ya Thika, polisi walikagua magari kwenye vizuizi walivyoweka karibu na Vincentian Retreat Centre, na hoteli ya Safari Park.

Kizuizi kingine kilikuwa karibu na uwanja wa michezo wa City kwenye barabara ya Jogoo.

Vizuizi kama hivyo viliwekwa katika barabara za Thika na Waiyaki. Mbali na kuweka vizuizi, polisi pia waliwakamata watu walioshuku kuwa waandamanaji katika barabara za Moi Avenue, Kenyatta Avenue, Kimathi, Mama Ngina, Uhuru miongoni mwa nyingine.

Washukiwa hao walikamatwa na polisi waliovalia kiraia ambao pia walitumia vitoa machozi kutawanya waandamanaji na kuwaamrisha watu kufunga biashara zao na kuondoka.

Polisi waliimarisha usalama katika majengo muhimu ya serikali kama vile Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Ikulu, Bunge, Afisi ya Rais na Benki Kuu ya Kenya. Mnamo Jumatano, Kaimu mkuu wa polisi Gilbert Masengeli alionya “wahalifu” walionuia kutumia maandamano hayo kupora na kuharibu mali. Bw Masengeli pia alionya waandamanaji kuepuka maeneo yaliyolindwa.

Kuanzia saa nane mchana, polisi walibadilisha mbinu kati ya jiji na kuagiza matatu na wanabodaboda wote kuondoka.

Baadhi ya wafanyabiashara walishtushwa na amri ya polisi waliowakamata waliposita kuitii.

Katika mji wa Kitengela, kwenye barabara kuu ya kuelekea Namanga, polisi waliwakamata waandamanaji waliojaribu kuwasha moto barabarani.

Maafisa wa kukabiliana na fujo waliweka kizuizi katika barabara ya Namanga kuzuia waandamanaji huku helikopta ikishika dora angani kufuatilia matukio katika eneo hilo.

Hatua ya polisi kufunga jiji ilitokana na tishio la waandamanaji kukusanyika kwa wingi na kukita kambi Nairobi kushinikiza mabadiliko serikakini.

Polisi wa kupambana na ghasia walikabiliana na vijana katika barabara za jiji. Magari mengi waliyotumia polisi yalikuwa yamefunikwa nambari za usajili ili yasitambuliwe.

Kupitia mitandao ya kijamii, vijana walikuwa wamehimizana kukusanyika jijini Nairobi kwa maandamano ya Nane Nane.

Licha ya usalama kuimarishwa na biashara zote kufungwa, vijana waliingia kati kati mwa jiji na kukabiliwa na polisi kwa vitoa machozi.

Vijana hao walizunguka kutoka barabara moja hadi nyingine huku polisi wakiwaandama kuzuia wasikusanyike au wavunje maduka na kupora mali.

Jana, kulikuwa na utulivu katika miji mingine nchini ambako maandamano yamekuwa yakifanyika kama vile Mombasa, Kilifi, Kwale, Nakuru, Karatina na Kisii.

Hata hivyo, polisi walipiga doria katika miji hiyo. Katika eneo la Makande, polisi walikagua magari yaliyokuwa yakiingia kati kati mwa mji wa Mombasa kutoka Changamwe na Nyali.

Shughuli za kawaida ziliendelea mjini Eldoret na Kisumu, Lamu na Makueni.

Ripoti za Dan Ogetta, Millicent Mwololo, Mercy Simiyu, Sammy Kimatu, Stanley Ngotho, Kalume Kazungu, Anthony Kitimo, Kevin Cheruiyot na Ndubi Moturi