Mbadi aanza kazi mara moja akitarajiwa kufufua uchumi
DAKIKA chache baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi alifufuliza moja kwa moja katika ofisi yake katika jumba la Treasury, Nairobi tayari kuchapa kazi.
Bw Mbadi alipokewa na makatibu wawili wa wizara hiyo Dkt Chris Kiptoo (wizara ya fedha) na James Muhati ( Mipango ya Uchumi) ambao walitumia muda kumfahamisha mkubwa wao mpya shughuli za wizara.
Baadaye Dkt Kiptoo na Bw Muhati walimtembeza waziri huyo katika afisi mbali mbali na kumtambulisha kwa wafanyakazi wa wizara.
Video ambayo Taifa Leo iliona inaonyesha Bw Mbadi, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama cha ODM akikaribishwa na wafanyakazi katika makao makuu ya Wizara ya Fedha.
“Tulimkaribisha kama kiongozi wetu na tukamhakikishia usaidizi na ushirikiano wetu,” alisema Dkt Kiptoo.
Mbadi ambaye ni mkaguzi wa hesabu aliyehitimu, na mmoja wa washirika wa kiongozi wa ODM Raila Odinga walioapishwa kuwa mawaziri Alhamisi alianza kazi ya uwaziri baada ya kuhudumu kama mbunge kwa miaka 18.
Washirika wengine wa Bw Odinga walioteuliwa mawaziri ni Bw Wycliffe Oparanya wa Wizara ya Ushirika, Hassan Joho wa Uchimbaji Madini na Opiyo Wandayi wa Kawi na Mafuta.
Kabla ya kuteuliwa waziri, alikuwa mbunge mteule na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uhasibu, inayochunguza masuala ya fedha.
Alianza kazi yake ya uhasibu katika Chuo Kikuu cha Nairobi alikokuwa mhasibu msaidizi kuanzia 1996, kulingana na wasifu kazi wake.
Mwaka wa 1999, alipandishwa cheo kuwa karani mkuu wa fedha, wadhifa ambao alihudumu hadi 2003 alipoajiriwa kama Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni ya Medair-Sudan Kusini.
Wasifu kazi wake unaonyesha kuwa Mbadi ana umilisi mkubwa wa masuala ya usimamizi wa fedha za umma, uhasibu, kupanga bajeti na ushuru miongoni mwa kazi zinazohusiana na fedha.
Bw Mbadi ambaye Bw Odinga alimtaja kama “mtaalamu” ana kibarua kigumu cha kufufua uchumi huku nchi ikilemewa na madeni na raia wakilia kubebeshwa mzigo wa ushuru.