Sina uwezo tena wa kutosheleza mwanamke chumbani- Louis Van Gaal
KOCHA wa zamani ambaye sasa ni mshauri wa klabu ya Ajax nchini Uholanzi, Louis van Gaal, 72, ametoa taarifa kuhusu jinsi anavyoendelea kupigana vita na saratani ya tezi dume.
Mkufunzi huyo wa zamani wa Barcelona, Bayern Munich na Manchester United aligunduliwa kuwa anaugua kansa mnamo 2021 lakini hapo awali akaweka hali yake ya afya kuwa siri.
Alishangaza wengi alipofunguka na kukiri kwamba alikuwa akipambana na ugonjwa wa saratani alipokuwa akiongoza timu ya taifa ya Uholanzi kwenye kampeni za Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.
“Nimekuwa nikiishi na ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka mitatu. Imekuwa ni kuchomwa sindano za homoni mara kwa mara, upasuaji mmoja baada ya mwingine na kubeba mifuko ya mkojo.”
“Huenda ninachosema kisiaminike, lakini ndivyo ambavyo hali imekuwa. Nimesimama nisianguke na niliweza kufanya kazi hata wakati wa fainali zilizopita za Kombe la Dunia,” akasema.
Kama ilivyo kwa mamilioni ya wanaume wanaougua saratani ya kibofu, korodani au tezi ya kiume kote ulimwenguni, utendaji wa kimsingi wa kibinadamu ambao hapo awali ulikuwa wa kawaida sasa ni shida pia kwa Van Gaal.
Alisema: “Ninaendelea vizuri. Baada ya miaka mitatu ya matibabu ya mionzi, maambukizo ya figo na upasuaji wa tezi dume, hatimaye ninaweza kuudhibiti ugonjwa huu.”
“Ninaweza kwenda haja ndogo kwa namna ya kawaida, na hilo ndilo jambo muhimu. Lakini siwezi kabisa kushiriki tendo la ndoa. Nimeuaga huo mchezo wa ngono na hilo huenda liwe tatizo kwa mke wangu Truus ambaye nilimuoa 2008.”
Hata hivyo, kuwa na saratani hakujabadilisha mtazamo wa Van Gaal kuhusu maisha.
“Tazama, ninatoka katika familia ambayo sisi ni ndugu tisa wa kiume. Mimi ndiye mdogo kwa wote. Babangu alifariki nikiwa na umri wa miaka 11. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 53.”
“Mke wangu wa kwanza, Fernanda Obbes, alifariki akiwa na umri wa miaka 39. Na ndugu zangu wote waliaga mapema sana. Nimezoea kifo na ninajua ni sehemu ya maisha.”
Alipoulizwa iwapo anaogopa kifo wakati wa mahojiano yake na wanahabari wiki hii, Van Gaal alijibu: “Kweli, mtu hafi haraka hivyo kutokana na saratani ya kibofu. Japo kuna baadhi ya watu wanaofariki kutokana na ugonjwa huo, wengi wao hufa kutokana na matatizo mengine. Sijaogopa sana, lakini sijapata maisha yangu yakiwa ya kufurahisha tena.”