Makamanda wapya wa Raila ODM
KIONGOZI wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga ameunda wadhifa wa ziada wa naibu kiongozi wa chama katika jaribio la kushughulikia maslahi ya kieneo, akijaza nafasi zilizoachwa wazi na washirika wake wakuu waliojiunga na Baraza la Mawaziri la Rais William Ruto.
Mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi ya ODM ulioongozwa na Bw Odinga mnamo Ijumaa ulipitisha kuwa Gavana wa Mombasa Abdullswamad Nassir, Gavana wa Kisii Simba Arati na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi kuwa Naibu wa kiongozi wa chama hicho cha chungwa.
Hapo awali, chama hicho kilikuwa na manaibu wawili wa kiongozi nyadhifa zilizoshikiliwa na waliokuwa magavana Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega). Chama kilikuwa kimeazimia kujaza nafasi zao na watu kutoka kaunti ambazo watatu hao wanatoka.
Lakini mikutano ya usiku na mivutano mikali iliyotangulia mkutano huo ilisababisha kubuniwa kwa wadhifa wa ziada uliomwendea Bw Arati baada ya viongozi jamii ya Gusii kulaumu chama hicho kwa kutenga eneo hilo baada ya kukosa nafasi tano za Baraza la Mawaziri zilizoendea Nyanza, Pwani, Magharibi na Turkana.
Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga ameteuliwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho, akichukua nafasi ya John Mbadi ambaye amejiunga na serikali kama Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi.
Bi Wanga aliungwa mkono na wabunge wengi wanawake wa ODM, waliotaka wanawake kujumuishwa katika ngazi za juu za uongozi wa chama.
Bi Wanga alikuwa ametangaza nia ya kugombea mojawapo ya nyadhifa za Naibu Kiongozi wa Chama. Ameelezea kufurahishwa kwake na nafasi ya Mwenyekiti wa Kitaifa, akisema kuwa ataanza kampeni kali ya kuleta wanawake na vijana wengi zaidi katika chama.
“Nimefurahi sana kupata nafasi hiyo muhimu. Sasa nitaanza kukifufua chama kwa kuleta wanawake na vijana wengi. Pia, nataka kumshukuru kiongozi wa chama kwa kuzingatia wanawake katika nyadhifa za juu za chama,” akasema Bi Wanga.
Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na mwenzake wa Turkana Kusini John Ariko walichaguliwa kuhudumu kama Makamu Wenyeviti wa chama huku Mbunge wa Kisumu Magharibi Rosa Buyu akichaguliwa kuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa wa chama hicho.
Wengine ni Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga kama Naibu Katibu Mratibu huku Rahab Robi, ambaye ni waziri wa serikali ya Kaunti ya Migori akiwa Katibu wa Masuala ya Umma na Habari. Mbunge wa Kajiado Mashariki Kakuta Maimai ndiye Katibu wa Mipango Maalum na Ustawi wa Jamii.
Katika taarifa yake, chama hicho kilisema Kamati Kuu Simamizi itatoa mapendekezo kwa Baraza Kuu ya Kitaifa ya chama na Baraza la Uongozi la Kitaifa ili kufanya mabadiliko muhimu ya Katiba ya chama kuzingatia mapendekezo ya nafasi tatu za naibu kiongozi wa chama.
“Kama mlivyoona, Kamati Kuu Simamizi imependekeza majina matatu ya Naibu Kiongozi wa Chama. Tutakuwa tukitoa pendekezo kwa NEC na NGC kufanya mabadiliko yanayofaa katika katiba yetu ili kuangazia haya,” alisema Bw Sifuna.
Bw Sifuna, Bw Nassir, Bi Wanga, Bw Ososti, Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na Gavana wa Busia Paul Otuoma ni baadhi ya vigogo waliokuwa wakimezea mate nyadhifa za Naibu Kiongozi wa Chama. Kikao hicho kilichoongozwa na Bw Odinga kinasemekana kuwa kiliamua Bw Sifuna kusalia Katibu Mkuu wa chama.
Maswali ya uaminifu kwa chama, hata hivyo, yaliibuka kuwahusu Bw Mung’aro na Bw Otuoma.
Bw Munga’aro aliwahi kuhama ODM na kurejea tu wakati wa uchaguzi uliopita huku Bw Otuoma akisemekana kuwa karibu na Rais Ruto hata kabla ya ushirikiano wa sasa wa kisiasa kati ya ODM na United Democratic Alliance (UDA).