Jamvi La SiasaMakala

Gachagua na Kiunjuri wapakana tope wakipigania ubabe Mlimani

Na MWANGI MUIRURI, BENSON MATHEKA August 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VITA vya ubabe kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri vimefikia kilele, kila mmoja akijitahidi kuangusha mwingine kisiasa.

Hivi majuzi, wawili hao wamekuwa wakizozana kuhusu jambo ambalo halijadhihirika waziwazi lakini linalojitokeza ni watu wawili wanaopigana vita vya kibinafsi.

Hata hivyo, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa hawajasahau kwamba Bw Kiunjuri aliwahi kuwa rafiki na mwanzilishi wa Grand National Union (GNU) akiwa na kaka mkubwa wa Bw Gachagua, marehemu Nderitu Gachagua ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa Nyeri.

Huku Bw Gachagua akiwa naibu kiongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Kiunjuri ana chama chake cha The Service Party (TSP).

Lakini Bw Gachagua si kinara mwenza wa muungano tawala wa Kenya Kwanza alivyo Bw Kiunjuri.

‘Vita vyao lazima viwe vya kibinafsi vilivyozuka miaka ya nyuma, au, kuhusu suala la ubabe wa kisiasa eneo la Mlima Kenya. Wote wawili wamehitimu kuwa wasemaji wa eneo hilo siku zijazo,’ alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Bw Charles. Mwangi.

Katika malumbano yao ya hivi majuzi, Bw Kiunjuri alimshutumu Bw Gachagua akidai alihusika kuchochea maandamano ya Gen Z dhidi ya serikali. Alidai Gachagua ni miongoni mwa waliofadhili wahuni 25,000 kusababisha ghasia.

Vile vile, alimshutumu Bw Gachagua kwa kumtusi Rais na kupanga jaribio la kumbandua uongozini.

Isitoshe Kiongozi wa TSP alidai kuwa Naibu Rais alitumia ukabila kwa nia ya kumnyima rais uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika misururu ya shutuma, Bw Kiunjuri amemlaumu Bw Gachagua akisema alimsumbua Rais hadi ikabidi ajumuishe washirika wa kinara wa upinzani Raila Odinga serikalini wamsaidie.

Huku Bw Gachagua na washirika wake wakidai hadharani kwamba anadhulumiwa na kuhujumiwa na watu walio karibu na rais, Bw Kiunjuri anadai shida zake nyingi ni za kujisababishia mwenyewe.

Bw Kiunjuri amekuwa akimpuuza Bw Gachagua na kumtaja kama mwanaharakati duni.

Mbunge huyo ambaye amesema kuwa ni lazima viongozi wa Mlima Kenya waanze kwa kuheshimiana, pia amemshambulia Bw Gachagua na washirika wake kuhusiana na madai waliyotoa wakiwa Kirinyaga Mei 19 2024.

Wakati huo, walimlaumu (Bw Kiunjuri) pamoja na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wakisema wao ni miongoni mwa wanaogawanya eneo hilo kisiasa.

Naibu Rais alitaja wanaompiga vita katika Mlima Kenya kama wasaliti na maadui wa wakazi wa eneo hilo kauli ambayo imemfanya Bw Kiunjuri kumshambulia vikali.

Alisema Bw Gachagua analazimisha viongozi kunyenyekea kwake kama watoto wa shule.

Baada ya Rais William Ruto kuvunja baraza lake la mawaziri na kuunda jipya lililojumuisha washirika sita wa Bw Odinga, Bw Kiunjuri alimlaumu Gachagua kwa kumsukuma rais kufanya uamuzi huo.

Alisema kwamba Mlima Kenya unapaswa kujilaumu kupitia Bw Gachagua kwa kutonyenyekea ndani ya serikali ambayo ulikuwa na mawaziri wengi.

Bw Gachagua alipuuza matamshi ya Kiunjuri kama ‘akili za kishenzi’ za watu wanaotumia maandamano kulipiza kisasi kwa watu wasiopenda.