Jamii yapinga kuuzwa kwa mashamba ya majani chai
JAMII ya Kipsigis imepinga mpango wa kuuza mashamba ya Liptons Teas na Infusion eneo la South Rift.
Kupitia Shirika la Koo za Jamii za Kipsigis, Wakipsigis wanadai uuzaji wa mashamba hayo ya chai katika kaunti za Kericho na Bomet haukufuata sheria wala kushirikisha wahusika wote.
Kampuni ya kimataifa ya Browns Investment Plc yenye makao yake nchini Sri Lanka ilikuwa ikisimamia mchakato huo.
“Tumewasiliana na mawakili na mamlaka husika. Tunakabili suala hili kwa misingi ya Kanuni Elekezi za Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara, na Haki za Binadamu za Jamii Asili,” shirika hilo lilisema.
Hatua yao ilifuatia taarifa ya kampuni ya Browns Investments Plc kwa Soko la Hisa la Colombo ya Agosti 2, 2024 kwamba shughuli ya kutwaa hisa za mashamba ya Lipton Teas and Infusions Kenya Plc ilikamilika Julai 30, 2024.
Katika taarifa iliyotolewa Agosti 7, 2024 mjini Kericho — ambayo ilitiwa saini na Mwenyekiti wa shirika hilo la kijamii Bw John Rop, Katibu Mkuu Bw Joel Kimetto na Mweka Hazina Bw Joseph Towett — waliapa kupambana liwe liwalo ili kubatilisha mchakato wa uuzaji mashamba hayo ya majani chai.
Shirika hilo linawakilisha wanajamii wa koo asilia za Kipsigis katika kaunti za Bomet, Kericho, Narok na Nakuru na pia nje ya nchi.
“Tuna ushahidi kwamba ombi la jamii kupewa mashamba hayo halikuzingatiwa. Aidha, mchakato wa uuzaji haukufuata utaratibu mwafaka wala kuendeshwa kwa uwazi,” shirika hilo lilieleza.
Linadai ardhi hiyo ilitwaliwa kwa nguvu kutoka kwa jamii ya Kipsigis kati ya 1902 na 1963 na serikali ya ukoloni ya Uingereza na kupewa walowezi wa Kizungu