Michezo

Afrika Kusini yadai Misri ilipendelewa kuandaa AFCON

January 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO 

SHIRIKISHO la soka la Afrika Kusini (SAFA) limelalamikia vikali jinsi mchakato mzima wa kuteua taifa la kuandaa fainali za nchi bingwa barani Afrika mwaka wa 2019(AFCON  2019) ulivyoendeshwa na Misri hatimaye kuteuliwa.

Afisa Mkuu wa Shirikisho hilo Russell Paul ameshutumu Shirikisho la soka barani Afrika(CAF) kwa kuendesha mchakato huo kibaguzi na kwa njia isiyo wazi.

“Sijahitimu kuzungumzia siasa ila nahisi kwamba jinsi suala hili lilivyoshughulikiwa lilichangia Misri kuteuliwa. Tangazo hilo lilitolewa siku moja kabla ya tarehe iliyokubaliwa na hatukujua na bado hatujui chochote kuihusu,” akatanguliza.

“Wamisri walikuwa na ujumbe wao wote na sisi tulikuwa tunapanga kufikisha ujumbe wetu huko  Dakar Senegal tarehe ya awali tuliyokubaliana. Tulishtuka sana kwamba uamuzi wa kupokeza Misri majukumu hayo ulikuwa umeafikiwa ilhali hatukuhusishwa,” akaongeza Paul.

Hata hivyo, afisa huyo alijinaki kwamba hakuna nchi inayojivunia miundombinu bora ya kuiwezesha kuandaa fainali hizo kama Afrika Kusini.

“Bila kuwasha moto hakuna nchi katika Bara hili ambayo ina vifaa na viwanja kama sisi. Njooni mcheze soka hapa hata usiku mjionee,” akahitimisha mkuu huyo wa soka ya Afrika Kusini.