Makala

Majirani Tanzania waambulia patupu, Kenya ikipata medali 11 Olimpiki ya Paris

Na LABAAN SHABAAN August 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeambulia patupu na haikuonekana kwenye orodha ya medali katika Mashindano ya Olimpiki Mjini Paris Ufaransa 2024.

Kulingana na rekodi ya maandalizi ya kufuzu, wanamichezo wanane wa Tanzania walikuwa na matumaini ya kuvaa nishani Jumapili.

Japo, matumaini yalionekana mbali na upeo wa macho yao siku zilipozidi kuyoyoma.

Wanamarathoni Magdalena Shauri na Jackline Sakilu walikuwa uwanjani kuwinda medali Jumapili Agosti 11, 2024.

Matumaini yao yaliyeyuka pindi mkimbiaji Mholanzi Sifan Hassan alipokata utepe na kuibuka mshindi.

Alifuatwa unyounyo na Muethiopia Tigst Assefa (nambari mbili) na Mkenya Hellen Obiri katika nambari ya tatu.

Awali katika mashindano, waogeleaji Collins Saliboko na Sophia Latiff, pamoja na mshiriki wa mchezo wa Judo, Andrew Mlugu, wote walitoka nunge bila kupanda jukwaa la medali.

Katika mbio za masafa marefu za wanaume Agosti 10, 2024, mtimkaji bora Tanzania Alphonce Simbu alikuwa namba 17.

Simbu alikuwa miongoni mwa waliopigiwa upatu kunyakua nishani. Mwenzake Gabriel Geay hakumaliza mashindano hayo baada ya kulemewa katikati.

Wakenya wasuta Majirani

Ukame wa kupata medali katika Olimpiki kwa Tanzania umedumu kwa zaidi ya miaka 40.

Kenya imezoa nishani 11, nne za dhahabu, mbili za fedha na tano za shaba.

“Jirani (akimaanisha Tanzania) hana medali. Anasoma tu kamusi akisikiza Mbosso (mwimbaji wa nyimbo za kizazi kipya Tanzania),” alitania mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii.

Mwingine akasema, “Kunavyoendelea, itabidi Tanzania ijiundie medali yake sasa.”

“Ni kama walienda kutalii tu,” mwengine akakejeli

Kikosi cha watu 18

Tanzania iliwakilishwa na watu 18 katika Olimpiki ya Paris 2024.

Walijumuisha watimkaji wanne wa marathon Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri, na Jackline Sakilu.

Wengine walioorodheshwa ni waogeleaji Collins Saliboko na Sophia Latiff, judoka Andrew Mlugu na bondia Yusuph Changalawe.

Orodha hiyo ilifungwa na kocha wanne, maafisa wa serikali, daktari na mwanahabari.

Medali mbili tu

Tanzania ilishiriki Olimpiki ikiwania medali telezi tangu 1980 katika makala ya Moscow, Urusi.

Tanzania ilishinda medali mbili katika historia ya Olimpiki. Medali hizi, zote za fedha, zilituzwa “majirani” katika mashindano ya Moscow.

Haijawahi kushinda nishani ya dhahabu ama hata shaba tangu ianze kushiriki mashindano mwaka wa 1964.

Walioshinda medali ni Suleiman Nyambui katika mbio za wanaume mita 5000 na Filbert Bayi aliyezoa nishani ya fedha katika mbio za wanaume mita 3000 kuruka viunzi na maji.